“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Februari 16 2021
Juma la 6 la Mwaka wa
Kanisa
Mwa 6: 5-8; 7: 1-5, 10;
Zab 29: 1-4, 9-10;
Mk 8: 14-21.
CHACHU
ULIMWENGUNI!
Karibuni ndugu zangu kwa
adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana, tafakari yetu
inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati: hapa tunakutana na
maneno yasemayo Bwana atawabariki watu wake kwa amani. Yeyote aliye na Bwana
anabarikiwa kwa amani.
Anayebarikiwa leo katika
masomo yetu ni Nuhu. Yeye basi alionekana kuwa mwema kati ya wanadamu wote wa
ulimwengu, hivyo anapokea baraka, anatunzwa na Mungu, anaamriwa atengeneze
safina itakayomkinga na maangamizi ya gharika. Nuhu hakufuata mkumbo wa
ulimwengu, hakuamua kwenda na wakati na kufikiri jinsi ulimwengu ulivyofikiri.
Hili lilimuokoa.
Sisi ndugu zangu
tujifunze kusoma alama za nyakati, tuachane na kasumba ya kuiga kila
kinachotendwa na ulimwengu. Ulimwengu haupaswi kutuongoza, sisi tuuongoze. Sisi
wakristo tunapaswa kuwa Nuhu wa vipindi vyetu. Hivyo itatubidi tuondoe kasumba
ya kutaka kunusa nusa kila kitu kitokacho ulimwenguni. Sio kila kitu kilichopo
ulimwenguni tujaribu kushiriki, si lazima niingie kila bar au kila aina ya
kumbi za starehe. Sio lazima ati ni nunue kila toleo jipya la simu au kwenda
tamasha la kila mwanamuziki. Dunia inahitaji Nuhu wa kutufundisha namna hii.
Ili tuwe Nuhu yafaaa
tuondokane na tamaa. Tudhibiti vionjo vyetu kila mara.
Kwenye somo la injili,
Yesu anawaambia wanafunzi wake wajiepushe na chachu ya Mafarisayo. Hawa
walikosa imani kwa Yesu, walimuonea Yesu wivu na kutaka asiheshimiwe na yeyote.
Walikuwa na chuki naye na utayari wa kumfanyia chochote kiovu. Kwa kitendo chao
cha kuanza kuona hofu kwa kutokuchukua mikate, yamaanisha kwamba bado walikosa
imani, walishindwa bado kuutambua ukuu wa nguvu yake.
Sisi tuishi kiimani,
tuwakubali wenzetu katika jamii waliojaliwa vipaji kuliko sisi. Tumtumainie
Mungu, tuombe abariki na yote tuyafanyayo. Atuepushe na chachu ya ukosefu wa
imani, tuishi tuwe imani siku zote, Amina.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment