“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumatatu
, Februari 22, 2021,
Juma
la 6 la Mwaka
SIKUKUU
YA UKULU WA MT. PETRO (MTUME)
1 Pt
5: 1-4;
Zab
23: 1-6;
Mt
16: 13-19.
MAMLAKA
YA KUTUMIKIA.
Karibuni ndugu zangu kwa
adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya ukulu
wa Mt. Petro. Hili ni adhimisho la cheo alichopewa huyu mtume na alikipewa na
Bwana mwenyewe mara tu baada ya kumkiri kwamba yeye ni Masiha Mwana wa Mungu
ajaye ulimwenguni. Yesu aliamua kumchagua mmoja kati ya wale mitume, awe halifa
wake kwa dunia hii. Yeye alipokea cheo na alivuviwa Roho Mtakatifu toka kwa
Yesu. Hiki ni cheo kikubwa sana. Cheo hiki ni ishara ya upendo toka kwa Yesu na
sasa kiko mikononi mwa Baba mtakatifu wetu. Na hivyo yapaswa tukiheshimu cheo
hiki.
Tafakari ya neno la Bwana
katika sikukuu hii linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka waraka wa mtume
Petro kwa watu wote. Hapa tunamkuta Petro akiwasihi wazee wenzake, mitume, na
maaskofu wa makanisa mbalimbali wawe waaminifu na walichunge lile kundi la
Mungu walilokabidhiwa na walichunge vyema.
Lengo ni hilo kundi
lifike kule Yesu alikoliitia. Petro alichukua jukumu hili la kuwaambia wazee
wenzake kwa sababu yeye alijua kwamba yeye alikuwa amechaguliwa kuwa kiongozi
wa lile kundi na hivyo ilikuwa ni jukumu lake kuangalia kwamba lile kundi
linafikia kule lilikotakiwa. Alijua kwamba uchu wa madaraka na uzembe wa
viongozi ungeliangusha lile kundi zima na hivyo ilimbidi alitilie maanani hili.
Katika injili, tunakutana
na Petro akimkiri Yesu kuwa Masiha. Wanafunzi wenzake hawakuwa na ujasiri wa
kumkiri Yesu kama Masiha lakini Petro aliweza. Na Yesu anamwambia Petro kwamba
ni Mungu mwenyewe ndiye aliyemwezesha, aliyemvuvia Roho ya kuweza kumkiri kama
Masiha miongoni mwa wanafunzi wake na kwa sababu hiyo, Yesu anamwahidia
makubwa, anamtakia heri na atakuwa Baba kiongozi wa mitume wote kama
tunavyosikia katika somo la kwanza na yeye atawashauri sana.
Ndugu zangu, katika
sikukuu hii, tunayo mengi ya kujifunza kama yafuatayo: kwanza, ni umuhimu wa
cheo cha Baba mtakatifu hapa duniani. Nafasi ya Petro sasa iko katika kiti cha
Baba mtakatifu. Yeye ni halifa wa Kristo na hivyo yafaa aheshimiwe na
kusikilizwa. Tusikilize mafundisho yake na nasaha zake anazotoa kila siku au
kila wakati wa matukio makuu makuu. Tusidharau kiti cha Baba mtakatifu. Sio
kiti cha kutunga bali ni Yesu mwenyewe alikiweka.
Halafu, kila mmoja lazima
akubali kuwa mwaminifu popote alipo ili awapatie mwongozo safi wakristo wenzake
wanaomtumainia hasa wale walio wadogo. Usimkwaze mtu ndugu yangu. Tuogope hili.
Petro anatusisitizia hili katika somo la kwanza.
Halafu, unapokuwa tayari
kusema ukweli juu ya mtu fulani, bila wivu au unafiki, Mungu atakubariki tu.
Yawezekana kwamba wale wanafunzi wenzake na Petro waliona kwamba kumwambia Yesu
kwamba ni Masiha basi itakuwa labda wanamkweza mno na ndio maana walikaa kimya.
Lakini yule aliyekuwa mkweli na mjasiri wa kusema ukweli hakika alibarikiwa.
Nasi tuwe wajasiri namna
hii ndugu zangu.
Tuwasheshimu viongozi
wetu wa dini. Na sisi viongozi wa dini tujitahidi kuwa mfano kwa lile kundi.
Tuache matendo yanayowakwaza wenzetu. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment