“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumatano,
Februari 3, 2021,
Juma
la 4 la Mwaka wa Kanisa
Ebr
12: 4-7;
Zab
103;
Mk
6: 1-6.
MAMBO
YA KAWAIDA YANATUFANYA TUWE TAYARI KUPOKEA YASIO YA KAWAIDA!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
zaburi yetu ya wimbo wa katikati, mwimbaji wa zaburi hii anatueleza kwamba
upendo wa Bwana ni wa milele kwa wale wanaomcha. Zaburi hii inatueleza kwamba
Bwana anapendezwa na wale wanaomcha, wanaompatia heshima ya pekee. Kumheshimu
Mungu hutufungulia mlango wa Baraka.
Somo
la kwanza linatueleza kwamba Bwana humletea magumu na mateso yule
anayempenda-lengo la mateso haya ni kutufundisha ili mpendwa wake apate
kuchukua tahadhari na kujifunza na kupata maarifa zaidi ya kuyafahamu maisha.
Hivyo, mwandishi wa kitabu cha Waraka kwa Waebrania anatutia moyo kwamba
tusonge mbele, tupige moyo konde na kujitia moyo pale tukutanapo na mateso.
Hapa
mwandishi anataka kutufundisha juu ya thamani kubwa iliyoko katika mateso. Kila
mateso lipo fundisho toka kwa Mwenyezi Mungu atakalo kutufundisha. Pia ipo
faida atakayotupatia zaidi. Sisi tuombe kutambua na kuiona faida iliyopo katika
mateso.
Wengi
tunashindwa kuivuna neema inayopatikana ndani yake. Ndani yake kuna fundisho
kubwa. Tusikubali teso lolote litupate bila kuona ujumbe Mungu anaotaka
kukuambia kupitia teso hilo.
Kwenye
somo la injili, watu wa nyumbani mwake Yesu wanapata nafasi ya kuhubiriwa
vizuri na Yesu. Yesu anafafanua neno vizuri. Lakini badala ya kumpokea ili awe
mwalimu wao na kumfaidi zaidi, wao wanamkataa kwa sababu anatokea familia ya
chini na wa palepale kijijini. Hivyo wanamkataa. Hivyo Yesu anakwenda
kuwafaidisha watu wa mataifa mengine na wao wanabaki bila kitu.
Sisi
tujifunze kuacha dharau. Dharau zimetufanya tushindwe kuiendeleza jamii. Wengi
wenye uwezo wameachwa na cha ajabu wanaochaguliwa ni wale wasio na uwezo yote
kwa sababu ya dharau. Mambo haya huirudisha jamii nyuma. Wanaoachwa wangekuwa
msaada zaidi kwa jamii. Tujifunze unyoofu nakupokea ujumbe wa kinabii ili tuweze
kuwa wema zaidi.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment