“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya Kwaresima
Jumamosi,
Febuari 20, 2021
Jumamosi
baada ya Jumatano ya majivu
Isa
58: 9-14;
Zab
86: 1-6;
Lk
5: 27-32
KUMTEMBELEA
DAKTARI WA MIOYO YETU!
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo masomo yetu
yanatuhimiza kutambua maovu yetu, kutakatifuza siku zetu zote kwa Bwana ili
tuweze kufaidi zaidi neema zitokazo kwa Bwana.
Nabii Isaya anawaeleza
wana wa Yuda kwamba njia ya Bwana wanaijua, wajibu wao wanautambua lakini
hawapati neema yoyote. Kosa lipo katika kuzembea na kukosa umakini katika mambo
ya Bwana. Uzembe ndio unaowafanya washindwe kuvuna neema toka kwa Bwana.
Walikuwa wakifanya vitu ili kutimiza ratiba tu.
Ndilo himizo tunaloambiwa
sisi pia katika siku ya leo. Wengi wetu tunasali, tunahudhuria misa za dominika
lakini hatupati mabadiliko. Yote haya yanasababishwa na uzembe, kutojali na
kuhudhuria kwa lengo la kutimiza ratiba tu. Tujitahidi tuepuke uzembe na
kufanya mambo kwa lengo la kutimiza ratiba. Haya yametufanya kuwa watu wa
kupoteza muda, kwa sababu hatuvuni chochote katika sala. Tuzidishe umakini
katika mambo yote ya sala. Tuepuke kumfanyia Mwenyezi Mungu maigizo.
Kwenye somo la injili,
Levi anaitwa na Yesu na anapokutana na Yesu, anabadili maisha yake, anakuwa
makini kuhusu mambo ya Mungu, anarudisha na alivyodhulumu. Hapa ndipo mlango wa
neema ulifunguliwa juu yake na maisha yake kubalika zaidi. Nasi tutambue kwamba
tutaionja neema ya Mungu maishani mwetu pale tu tutakapokuwa makini na mambo ya
Mungu, kurudisha tulichodhulumu, na kumkaribisha Yesu nyumbani mwetu kama
anavyofanya Levi katika injili.
Na hapa ndipo milango ya
neema itakapofunguliwa juu yetu na hakika tutaweza kufurahia zaidi baraka na
neema zake.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment