“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumanne,
Februari 9, 2021,
Juma
la 5 la Mwaka wa Kanisa
Mwa
1:20 - 2:4;
Zab
8: 4-9;
Mk
7: 1-13.
KENGELE
YA KANISA!
Karibuni ndugu zangu kwa
tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo
zaburi yetu ya wimbo wa katikati ni zaburi ya 8 “jinsi lilivyotukufu jina lako
ulimwenguni kote Ee Bwana.” Hii ni zaburi ya Daudi inayotukuza uumbaji. Inashangilia
jinsi uumbaji unavyomtangaza Mwenyezi Mungu. Pia inatambua jinsi mwanadamu
alivyopewa hadhi na Mwenyezi Mungu, hadhi ya kutawala na kuvihudumia viumbe
vingine. Pia inatambua thamani ya kila kiumbe-hata kachanga “wasifika na vinywa
vya watoto wadogo na wanyonyao.” Kila kiumbe kina hadhi pekee mbele ya Mungu.
Zaburi hii inatumika
kutilia mkazo ujumbe wa uumbaji katika somo la kwanza. Leo tunasikia juu ya
uumbaji wa mwanadamu na jinsi anavyokabidhiwa kuvitunza viumbe vingine.
Tunakabidhiwa jukumu la kuutunza ulimwengu wote. Tukiwa ulimwenguni sisi ni
mawakili wa Mungu. Hivyo tutambue wajibu wetu, tuwe watu wa kuvipenda viumbe,
tusifurahie vikiteseka. Sisi tutambue kwamba ni wamawakili wa Mungu hapa ulimwenguni.
Katika somo la injili,
Yesu anawaambia Wafarisayo kwamba ni lazima waanguke miguuni mwa Mungu ili
wapate kufundishwa sheria za Mungu. Ukosefu wa unyenyekevu wa namna hii
uliwafanya washindwe kuzitambua sheria za Mungu, wakaishia kutunga zao ambazo
haziwezi kuwapatia wokovu.
Sisi tutambue kwamba ni
viumbe vya Bwana. Ni lazima tuwe watu wa kuanguka miguuni pa Mwenyezi Mungu
kuomba msaada wa nguvu zake, tumwambie Bwana nioneshe sheria zako, ili kwa njia
ya hizi tuweze kupata wokovu.
Huu ndio unyenyekevu
unaohitajika mbele ya Mungu. Sisi ni viumbe vyake, tuwe na utayari wa kuanguka
miguuni mwake. Tusipokuwa watu wa kuanguka miguuni pake, hakika tutakuwa
tunatwanga maji katika kinu. Ndicho walichofanya mafarisayo. Hawakumuomba Mungu
awafundishe sheria zake. Wakawa wanajitahidi kila siku kufanya kazi ya Bwana
lakini wakashindwa tu.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment