Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

JE UNA NJAA YA MUNGU?

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya kila siku

Jumamosi, Februari 13, 2021,

Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa

 

Mwa 3:9-24;

Zab 90: 2-6, 12-13;

Mk 8: 1-10.

 

JE UNA NJAA YA MUNGU?

 

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika ashimisho la Misa Takatifu. Neno la Bwana leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na maneno yasemayo “Ee Bwana umekuwa msaada wetu kizazi hata kizazi.” Kabla hata ya misingi ya dunia kuumbwa huyu Bwana amekuwa msaada wetu. Na akimueleza mwanadamu siku zake zimekwisha, yeye hurudi mavumbini alimotoka. Hivyo mwanadamu anapaswa aishi kinyenyekevu mbele ya Bwana kwani hatma yake ipo mikononi mwa Bwana.

 

Zaburi hii inatumika kusisitizia kwa undani ujumbe wa somo la kwanza. Hapa mwanadamu anadanganywa na kupewa adhabu kali. Adhabu hii lengo lake ni kumnyenyekesha, ajue nafasi yake ili apate kurudi kwa Mungu, amtumainie Mungu zaidi, akae miguuni kwa Mungu. Kwa namna hii, mwanadamu ataweza tena kupokea baraka na neema toka kwa Mwenyezi Mungu na kubarikiwa. Hivyo, adhabu hii isitufanye tuhuzunike sana, hii ni adhabu ya kutufanya tumrudie Mungu, tuanguke miguuni mwake, tujue kwamba bila yeye sisi si kitu. Hivyo tumpatie Mungu utukufu wake, tupige magoti, tumueleze kwamba bila wewe sisi si kitu, twende kwake kila siku kuomba huruma yake. Tumtumainie.

Katika somo la injili, tunakutana na Yesu akiwalisha makutano chakula. Yesu anajionesha kuwa Baba wa huruma, anawaonea wengi huruma, anajali hata mahitaji yao ya mwili. Alionesha kujali zaidi kabisa ya wanafunzi wake. Ukweli ni kwamba Yesu ajua shida zetu zaidi, pia tutambue kwamba kabla ya Yesu kuwalisha, aliwaeleza waeleze walichonacho, na pale walipokitoa alikibariki na kuwafanya wengi wale na kushiba.

 

Sisi tujapo kwa Bwana, lazima tukubali kuonesha sehemu yetu, twende na juhudi yetu ili Bwana azibariki na hapa atatuwezesha kupata na kushiba. Wengi wetu ni maskini kwa sababu hatuoneshi sehemu yetu, hatuoneshi sehemu yetu kwa Bwana, tunataka yeye atufanyie kila kitu bila kuonesha sehemu yetu. Hii ni sababu ya wengi wetu kushindwa kupata kile tuombacho. Ni lazima kukubali kuonesha kilicho chetu mbele ya Bwana. Tukionesha uvivu na uchoyo hakika hatutaweza kufaulu mbele ya Bwana.

 

------------------------

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

 

No comments:

Post a Comment