“ASALI
MUBASHARA”
Januari
4, 2021.
------------------
Jumatatu,
baada ya Epifania
1Yoh.
3:22-4:6
Mt.
4:12-17, 23-25
Karibuni
ndugu zangu katika dhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo tunachojifunza
katika masomo yetu ni kwamba tamaa hukwamisha utume wa Bwana.
Leo
neno la Bwana katika somo la injili, tunamkuta Yesu akianza kazi yake ya
umasiha. Anajitokeza mtaani na moja kwa moja anakwenda kwa wale wanaoteseka,
anahubiri habari njema huko na kuponya na kutoa matumaini. Injili hii
inatuambia kwamba Yesu anaanza utume wake katika Galilaya ya mataifa, eneo
lililodharaulika, lenye watu wengi wasio na mchungaji. Yesu anaanzia hapo.
Ndipo atakachopochagua na mitume wake na kufanya miujiza mingi.
Eneo
hili lilikuwa na njaa ya kuhubiriwa habari njema. Yesu aliamua kwenda kwenye
eneo la watu wa chini. Sisi nasi tutambue kwamba utume wa kanisa lazima ulenge
watu wa chini, usiwatekeleze, uwapatie nafasi. Lakini cha ajabu kipindi chetu
ni tofauti. Wengi tunangangania utume kwa sehemu za watu wa juu. Sehemu za
matajiri zina watumishi wengi sana kiasi kwamba wengine hawahitajiki. Sehemu za
watu wa chini hakuna kitu. Hata watu wa chini wenyewe wanaacha kufanya utume
kwenye yale maeneo yao wanakwenda ati kule kwa watu wa juu. Tuache kuweka
maslahi binafsi mbele.
Yesu
hakuweka maslahi binafsi mbele. Tuone huruma ni kwa namna gani kuendekeza kwetu
tamaa kumewaacha maskini wengi bila kulisikia neno la Mungu na kuishia kuishi
tu hivihivi-namna gani tamaa zangu zinavyorudisha utume wa Kristo nyuma. Kazi
ya Kristo isifanywe kwa tamaa bali kwa moyo safi kabisa.
Somo
la kwanza linakumbushia juu ya uwepo wa manabii wengi wa uongo. Wengi tunakuwa
manabii wa uongo kwa sababu ya tamaa na kuigeuza injili ya Kristo. Tunaigeuza
injili ya Kristo na kuifanya iseme kile tunachotaka kusikia au kuona ambacho
kinaendana na maslahi yetu na mategemeo yetu.
Mahali
pengi injili ya Kristo inatafsiriwa kiajabu. Yote haya ni kutokana na
kutanguliza tamaa mbele. Tutambue kwamba tamaa mbele mauti nyuma.
Hatutabarikiwa kwa kuigeuza geuza injili ya Kristo kiajabu ajabu hivi. Ni lazima
tufikie mahali tuwe wakweli na kuipatia injili hii tafsiri sahihi. Tumsifu Yesu
Kristo.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment