“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Ijumaa,
Januari 29, 2021,
Juma
la 3 la Mwaka wa Kanisa
Ebr
10: 32-39;
Zab
37: 3-6, 23-24, 39-40;
Mk
4: 26-34
MBEGU
ZA UFALME WA MUNGU!
Ndugu
zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo.Wokovu wa wenye
haki watoka kwa Bwana. Huu ni ujumbe wa zaburi yetu ya wimbo wa katikati.
Inasisitiza kwamba Bwana humlinda mwenye haki, humpatia wokovu. Wokovu wa
yeyote mwenye haki upo kwa Bwana.
Hivyo
mzaburi anawatia moyo waamini wazidi kumwamini Bwana. Hakika hatawaacha bila
kuwakumbuka. Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambapo
mwandishi wa barua kwa Waebrania anawaeleza kwamba yawabidi wabakie katika
imani. Wao ni watu wa imani na kuna kipindi kilipowabidi kuteseka kwa sababu ya
imani yao. Hili lipo lakini hakika Bwana hatawaacha. Hivyo wasikatishwe tamaa
na maumivu au masengenyo wanayoyapata. Bwana atawakumbuka na hataacha kuwapatia
wokovu.
Ujumbe
huu ututie moyo na sisi ndugu zangu kwamba ipo siku tutafurahia pamoja na
Bwana-ipo siku machozi yetu na maumivu yetu, mahangaiko na wasiwasi wetu
zitafikia mwisho. Ipo siku. Hivyo tujipe moyo. Wale tulio wagonjwa tufarijiwe
na neno hili. Na wale tunaowatunza wagonjwa wetu pia tufarijiwe na neno hili.
Litufariji na baadhi yetu pia ambao tunafanya kazi zenye kuchosha kweli kiasi
kwamba miili yetu hubakia hoi kila siku. Tufarijiwe na neno hili.
Kwenye
somo la injili, Yesu anaelezea ufalme wa mbinguni kama ufalme ambao upo ili
ukue-na si udidimie. Upo kwa ajili ya watu, na unasubiria watu wajiunge ndani.
Mfano wa kwanza unatuambia kwamba ufalme huu tayari una nyenzo zake za kuufanya
ukue. Kila nguvu na neema zipo ndani yake. Ni juu yam mea au mwanadamu kutumia
vile virutubisho vilivyoko. Sisi wakristo tutumie sakramenti zetu vyema na
viongozi wetu ili tupate kukua.
Mfano
wa pili unaonesha kwamba ufalme huu huanzia katika mambo madogo na kuishia kuwa
makubwa. Yote haya yanawezekana kutokana na neema ipatikanayo ndani ya ufalme
huu. Sisi tushirikiane na neema iliyo ndani ya huu ufalme na hakika tutafika
mbali. Katika udogo wetu na umaskini wetu-tukishirikiana na Bwana, twaweza
kufanya makubwa. Tuache tabia za kusingizia umaskini na mwishowe kuishia bila
kufanya chochote. Huku ni kuchezea neema ya Bwana.
Hakuna
aliyepewa kidogo sana ambacho Mungu hajalenga kiwe kikubwa. Sisi tusikubali
kudumaza yale madogo aliotupatia Mungu. Anatuhitaji tuyakuze kwa maisha yetu na
kuwa makubwa kwa kujenga ufalme wake.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment