“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Januari
6 2021.
------------------------------------------------
JUMATANO,
BAADA YA EPIFANIA
1
Yn 4:11-18;
Zab
72: 1-2, 10, 12-13;
Mk
6: 45-52.
KUTULIZA
DHORUBA KATIKA MAISHA YETU!
Karibuni
sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo
neno la Bwana tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la injili. Hapa
tunakutana na wanafunzi wakiwa wenyewe kwenye bahari wakitaabika na dhoruba
kali na mawimbi. Na majaribu haya wanayapata tena baada ya kuona muujiza mkubwa
wa Bwana Yesu, muujiza wa kuwalisha watu maelfu.
Baada
ya muujiza huu tu wanadumbukia kwenye majaribu ya kuteswa na mawimbi baharini
kiasi cha kukata tamaa. Ule muujiza walioonyeshwa na Yesu wa kuweza kuwalisha
maelfu ya watu ungalipaswa kuwaongezea imani kipindi hiki cha majaribu
baharini. Lakini wao inaonekana hawakusaidiwa na ule muujiza, waliishia kuogopa
na kusahau kila kitu na hata Yesu alipofika kwao, walishindwa kumtambua
wakafikiri kwamba ni lipepo limewajia kuwaongezea shida tena.
Sisi
nasi ndugu zangu huwa tunaonyweshwa miujiza na Bwana kila siku. Upo wakati
Mungu anakusaidia. Sasa, ikifika wakati ule wa shida au majaribu, tunapaswa
kusaidiwa na yale matumaini tuliyoonywesha na Bwana kipindi kile cha msaada.
Tukiruhusu kutawaliwa na vipindi vya matatizo, tutashindwa kusaidika, hata
Bwana akija kwetu tutamchanganya tudhanie kwamba bado ni mzimu tu.
Basi
tuzidi kumuita Bwana hata wakati wa matatizo, tusitumie nguvu zetu tu kama hawa
wanafunzi. Akija kwetu hata muda wa kufanya kitu unapungua. Wengi tunafanya
vitu kwa muda mrefu kama hawa wanafunzi kwa sababu ya ukosefu wa Bwana.
Kwenye
somo la kwanza tunaelezwa kwamba Mungu ni upendo nasi yatupasa kuwapenda
wenzetu. Binadamu ni viumbe vya Mungu. Hata kama sisi tutavichukia, Mungu
atazidi kuvipenda. Hatuwezi kumzuia Mungu asivipende. Tuache tabia za
kuwachukia watu bila sababu, au tabia za kuwatazama wenzetu kwa macho ya hasira
na chuki. Hata tukiwaangalia kwa macho ya chuki vipi, hakika watazidi kupendwa
tu na Bwana. Bwana hawezi kuwaacha na hatutaweza kuzuia riziki zao. Tuache
macho yenye chuki kwa wenzetu.
-------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment