Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUMTAFUTA YESU KWA MOYO WOTE!

 

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Alhamisi, Januari 14, 2021,

Juma la 1 la Mwaka wa Kanisa

 

Ebr 3: 7-14;

Zab 94: 6-11;

Mk 1: 40-45

 

 

KUMTAFUTA YESU KWA MOYO WOTE!

 

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo, ujumbe mkuu wa leo ni 'Msiifanye Migumu mioyo yenu'.

 

Leo kwenye somo la kwanza, mwandishi anasisitiza kwamba tusiifanye migumu mioyo yetu kamwe mbele ya Mwenyezi Mungu; yaani tusiwe watu wa kiburi, watu wanaotendewa miujiza na Mwenyezi Mungu bila kuruhusu miujiza hiyo itubadilishe; watu tunalishwa sakramenti kila siku lakini hazitubadilishi. Kwa sababu tunaifanya migumu mioyo yetu.

 

Mzaburi wetu katika wimbo wa katikati leo anatupatia mfano wa walioifanya migumu mioyo yao. Hawa ni wazee wa Israeli kule jangwani. Walioonyeshwa miujiza mikubwa na Mungu, wakalishwa mana na kunywa maji katika mwamba. Mungu akawapigania, akawaongoza kwa nguzo ya moto usiku na wingu mchana. Akawaokoa na mataifa mabaya lakini wao wakaendelea kuwa wakaidi. Wakakosa imani, wakadiriki hata kutengeneza sanamu na kuiabudu kama Mungu. Mungu alikasirika sana na kuwapa adhabu kubwa.

 

Sisi tusiige mifano ya babu zetu hawa. Turuhusu Mungu azungumze nasi, halafu tuwe tayari kumwona Mungu kwenye matukio mbalimbali maishani mwetu. Kuna wakati Mungu anatutendeaga miujiza-kuna mambo yanatutukia na tunaona kwamba hakika huu ni mkono wa Mungu. Matukio kama haya yanapaswa kutubadilisha. Tusikaze mioyo na kuona kana kwamba hakuna kitu kimetokea.

 

Mkoma tunayekutana naye katika injili ya leo alionyesha unyenyekevu, aliufungua moyo wake, hakuufanya kuwa mgumu na kwenda kwa Yesu na kweli aliponywa. Yesu anawapenda wasioifanya migumu mioyo yao. Tukumbuke kwamba waliokuwa na ukoma ni wengi nyakati za Yesu lakini walioponywa ni wachache. Waliokuwa na unyenyekevu kama wa huyu mkoma wa leo walifaidi. Sisi tuepuke kuifanya migumu mioyo yetu. Tuungame pia na dhambi zetu. Hizi hufanya mioyo yetu kuwa migumu na kushindwa kuona nguvu ya Mungu ndani yetu. Tuikimbie dhambi!

 

Copyright ©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment