“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi,
Januari 09, 2021,
Juma
baada ya Epifania
1
Yoh 5:14-21;
Zab
149: 1-6,9;
Yn
3:22-30.
KUBAKI
DAIMA KWAKULITAZAMA FUMBO LA NOELI
Karibuni
ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo katika injili
yetu tunakutana na Yohane akikiri waziwazi kwamba yeye sio Masiha na kwamba
yeye ni lazima azidi kushuka na Yesu kupanda. Anatambua nafasi yake kama
mpambe, kama anayekuja kuandaa njia kwa ajili ya mkuu wake.
Ama
kweli Yohane alijitambua na kujikubali na kuipenda nafasi hii yake kama mpambe
tu wa Bwana Yesu. Ni wachache wenye ujasiri wa namna hii. Wengi wetu hatuko
tayari kujitambulisha kama mke au mume wa mtu fulani, au kama mfanyakazi wa mtu
fulani kwa sababu ya kufikiri kwamba tukifanya hivyo tunajidhalilisha. Na mara
nyingi tumeishia kuingilia maamuzi yaliyo juu yetu na tukaishia kuharibu. Na
mbaya zaidi tupo ambao tumeona aibu hata kujitambulisha kama wafuasi wa Bwana.
Tukafika maeneo fulani tukaona aibu hata kufanya ishara ya msalaba, au kuvaa
hata msalaba au hata kusali.
Yote
haya yanatokana na ukosefu wa kujitambua, ndio maana tunamuonea hata Mungu
aibu. Ndio maana tumeingilia hata maamuzi ya wakubwa zetu, na ndio maana
tumewakana hata wazazi, waalimu, dini, wake na waume zetu. Baadhi yetu
tumeishia kugombania madaraka yasiyo yetu kutokana na kutokujitambua na
kukubali hali yetu. Kila mmoja wetu amwombe Mungu ili basi aweze kujitambua na
kufanya yampasayo.
Somo
la kwanza linatueleza kwamba ikiwa tutaomba chochote ambacho kinaendana na
matakwa ya Bwana hakika tutakipokea. Wengi wetu tunasali bila kupata kwa sababu
tunaomba vilivyo kinyume na matakwa ya Bwana. Tunaomba ili tukawe mabosi;
tuwatawale wengine. Wengine tunaomba vitu ambavyo tunajua hatuna uwezo wa
kuvifanya lakini tunangangania. Yote haya ni ukosefu wa kujitambua. Tutambue
hali yetu nasi hakika tutaweza kumpendezesha Bwana.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment