“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Desemba
29, 2020.
------------------------------------------------
JUMANNE,
OKTAVA YA NOELI
Somo
la 1: 1Yn 2: 3-11 Yohane anatuambia kwamba hatuwezi kumfahamu Yesu hadi
tumeshika amri zake: kumpenda Mungu na jirani.
Wimbo
wa katikati: Zab 95: 1-3,5-6 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, tangazeni wokovu wake
siku kwa siku na maajabu yake kati ya watu.
Injili:
Lk 2: 22-35 Luka anatuambia kuhusu kutolewa kwa mtoto Yesu hekaluni, na Simeon
anatabiri kwamba upanga utapenya katika moyo wa Maria Mama yake Yesu.
------------------------------------------------
UWEPO
WA MUNGU KATI YETU!
Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la
Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la injili
tunakutana na Mzee Simeoni akishangilia baada ya kukutana na Bwana. Anayo kila
sababu ya kufurahi kwa sababu ni kitu alichokisubiria kwa maisha yake yote na
leo amekipata. Ameweza kukutana ya yule aliyetegemeo na mwanga wa mataifa.
Hivyo basi aliona maisha yake kukamilika. Aliona kwamba Kristo amemletea mengi
sana na hivyo akawa na kila sababu ya kufurahi.
Sisi ndugu zangu tunapaswa kuonesha furaha
kama hii ya Simeoni. Tutambue kwamba maisha yetu yanafikia ukamilifu kwa
kukutana na Yesu, bila Yesu aliona kupungukiwa. Kukutana na Yesu aliona maisha
yake kufikia ukamilifu.
Nasi tunapaswa kuwa na hamu kama hii
aliyokuwa nayo Simeoni. Lazima tujione kwamba tumepungukiwa, kwamba bila Yesu
hatujafikia ukamilifu bado. Hata tunapokuja kanisani, lazima tuone kwamba bila
ile Ekaristi bado hatujakamilika.
Tamaa ya namna hii ndiyo itakayoweza
kutubadilisha na kutufanya tuone umuhimu wa Yesu maishani mwetu. Mioyo yetu
lazima iandaliwe kama wa simeoni, yeye muda wote alikuwa akienda hekaluni
akitegemea kwamba labda atakutana naye. Nasi tuwe na maandalizi ya namna hii
pia na hakika tutaweza kuiona nguvu ya Kristo maishani mwetu.
Basi ndugu zangu tusisahau kujitayarisha
kwa mapokezi ya Bwana wetu na hasa kwa kuwapenda wenzetu kama Yohane
anavyosisitiza kwenye somo la kwanza. Tuache kuwachukia watu bila sababu, wao
ni viumbe vitakatifu vya Mungu. Tutembee nao, tuwasaidie katika shida, na
tuondoe chuki kwa wengine bila sababu. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment