MASOMO YA MISA DESEMBA 29, 2020
SIKU YA TANO YA OKTAVA YA KUZALIWA BWANA
SOMO 1
1Yoh. 2:3-11
Wapenzi, Na katika hili twajua ya kuwa
tumemjua Yesu, ikiwa tunashika amri zake, Yeye asemaye, Nimemjua, wala
hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye
alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.
Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani
yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.
Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ila amri
ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile
mlilolisikia.
Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo
kweli ndani yake na yenu; kwa kuwa giza linapita na vile nuru ya kweli
imekwisha kung’aa. Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake,
yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani
yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena
anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza limempofusha macho.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1-3,5-6 (K) 11a
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote,
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. (K)
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku,
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu,
Heshima na adhama ziko mbele yake,
Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu
pake. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Siku takatifu imetung’aria: Enyi mataifa,
njoni mkamwabudu Bwana: Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.
INJILI
Lk. 2:22-35
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika
kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda na Yesu hata Yerusalemu, wamweke
kwa Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe
mtakatifu kwa Bwana, wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya
Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.
Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na
mtu, jina lake Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu
mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu
alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona
mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho;
na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa
desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu,
akisema, Sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa Amani kama ulivyosema kwa
kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote;
nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
Na babaye na mamaye walikuwa
wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki akawaambia
Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinua wengi walio
katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Naye mwenyewe, upanga utaingia
moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment