“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Desemba 9, 2020.
JUMATANO, JUMA LA 2 LA
MAJILIO
Somo la 1: Isa 40: 25-31
Mungu anajifunua mwenyewe kama Mwenyezi, anayefahamu yote, na bado anawajali
watoto wake, wale wote wanao mtumaini hawata tikisika wala kuwa na hofu.
Wimbo wa katikati: Zab
102: 1-4, 8, 10 Moyo wangu wamtukuza Bwana kwani ni yeye mwenyewe anayesamehe
udhaifu wetu, anaye okoa maisha yetu kutoka katika kaburi, anaye kuvika kwa upendo
na huruma.
Injili: Mt 11: 28-30 Yesu
anatualika sote tumuendee, tuchukue nira yake na kujifunza kwake, kwani ni
mpole na mnyenyekevu wa moyo.
------------------------------------------------
TUKABIDHI MIZIGO YETU
TUPATE PUMZIKO KWA YESU!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo na leo masomo yetu
yanaongozwa na maada ya kuwa, Bwana ni Mwenye Uwezo Mkubwa, Mtumainie.
Somo
la kwanza wana wa Israeli wapo nchini Babuloni na wanashangazwa na sifa
anazopewa huyu Marduku, mungu wa Babuloni na watu wake. Wao walimtangaza
Marduku kama Mkuu, aliyewawezesha hata kuwakamata mateka wana wa Israeli.
Hivyo, walimtangaza Marduku kuwa mkuu zaidi ya Bwana Mungu wa Israeli. Wana wa
Israeli waliposikia habari hizo-na kuangalia maendeleo ya wana wa Babuloni,
waliogopa, wakanywea, wakidiriki hata kukosa imani.
Leo
Isaya anawaeleza kwamba Mtumainieni Mungu, Mungu wetu ni mwenye uwezo mkuu,
yeye ndiye aliyeifanya dunia na kuiweka mahali pake, ni yeye tu awezaye hili.
Hakuna zaidi yake.
Sisi
nasi tunamhitaji Isaya mwingine aje atutie nguvu. Wengi wetu tumekata tamaa,
hatuoni tena kwamba Mungu ana nguvu tena, tukitishiwa na ushirikina kidogo tu
tayari tunaogopa ajabu, au ukitishiwa na mwenye pesa kidogo tu, tayari unaogopa
na kukosa amani, au msichana akiona umri unapita bila ya yeye kuolewa yaani
anaogopa anakuwa tayari hata kubadili dini ajiuze tu kwa mtu wa dini tofauti.
Mwingine akiishiwa pesa hapo mfukoni ataogopa ajabu.
Sisi
ndugu hatupaswi kuogopa hivyo, Mungu wetu ana nguvu za ajabu, sio wa kutishiwa
na vitu vidogo kama hivi. Tunafanya haya kwa sababu hatuujui ukuu wa nguvu za
Mwenyezi Mungu. Sisi tumtegemee Bwana, hakika tusiwe watu wa kutishiwa na mambo
madogo na kukosa amani.
Somo
la injili tunaalikwa tupeleke masumbuko yetu kwa Bwana. Haya ni maneno yaliyojaa
furaha kubwa. Ni wangapi wanaofarijiwa na Bwana? Lakini nakueleza, mimi kwenye
tafakari zangu naona kwamba kama ingekuwa tumekwishalikumbatia fundisho hili,
tusingalisumbuka namna hii ndugu zangu. Tubadilike. Ulimwenguni tunahitaji
kufarijiwa na Bwana na bila hili hatutaweza kusonga mbele.
Kuna
majanga na mapito mengi mno. Siku itakuja ambapo utajisikia mambo hayaendi
kabisa, unaona maisha hayana maana, hata ulichojitahidi kulima au kujiwekea
akiba hakina maana. Kweli hapa ndipo utakapoona umuhimu wa Bwana. Bila Bwana
mwanadamu hawezi kusonga mbele. Asante ee Bwana kwa kukubali kuwa nasi.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment