“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Desemba 28, 2020.
------------------------------------------------
JUAMTATU, OKTAVA YA NOELI
Sikukuu ya Watoto Mashahidi,
Somo la 1: 1Yn 1:5 – 2:2 Yohana anatuambia
kwamba sisi ni wakosefu tunamuhitaji Kristo. Jitihada yake kubwa ni kutusaidia
sisi tuwe mbali na dhambi.
Wimbo wa Katikati: Zab 123:2-5,7-8 Maisha
yetu, kama ndege, yameokoka katika mtego wa wawindaji, kwani msaada wetu upo
katika jina la Bwana aliyeumba mbingu na nchi.
Injili: Mt 2: 13-18 Mathayo analinganisha
kwenda kwa mtoto Yesu Misri na mauaji ya watoto wachanga-watoto wote wa kiumbe
wenye umri chini ya miaka miwili. Hawa watoto watakatifu waliuwawa kwasababu ya
Kristo. Walimfuata Mwanakondoo asiye na hatia, na kutangaza milele utukufu wa
Bwana.
------------------------------------------------
MUNGU ANAWEZA KUFANYA MAMBO YOTE KUWA
MAPYA!
Karibu ndugu zangu katika adhimisho la
misa Takatifu, leo tuna adhimisha sikukuu ya Watakatifu Watoto Mashahidi: hawa
tunasikia habari zao katika injili ya leo. Wanauawa kwa ajili ya Kristo bila
hatia na Herode aliyetaka kulinda ufalme wake. Mtoto aliyehofiwa alikuwa mmoja
tu lakini hofu yake inapelekea kuuawa kwa watoto wasiofahamu hata maana ya
ufalme. Yote haya ni kwa sababu ya uchu wa madaraka.
Lakini siku zote uovu hauwezi kuushinda
wema. Yesu aliokolewa na kupelekwa Misri na hivyo ufalme wake ulizidi kubakia.
Herode alikufa muda mfupi baadaye na kupoteza ufalme. Alipokufa alikuta watoto
aliowateketeza kama wafalme-mashahidi mbinguni wakikalia viti kumi na viwili na
kuwahukumu makabila yote kumi na mbili ya Israeli (Mt 19:28). Hivyo,
kumshuhudia Yesu hakuna umri, jinsia au rika. Awe mtoto au mzee anapaswa
kumshuhudia Yesu.
Kingine ndugu zangu nyakati zetu tunaweza
kuwa na Maherode wengi wanao winda roho za watoto wachanga wakiwa tumboni mwa
Mama zao na kuwatoa mimba. Yaweza kuwa wanafanya hivyo kwa hofu ya kuogopa
kuitwa Mama au kupoteza uzuri wake kwani atanyonyesha na watu watafahamu kwamba
sasa ana mtoto na hivyo hatapata tena wanaume wakumpenda. Hawa hawana tofauti
sana na Herode, tunaweza kumlaumu Herodi lakini pengine sisi wenyewe ni
Maherode, wale wanaouza dawa za kutolea mimba, wenye kushauri watu watoe mimba,
wazazi wanaotoa mimba kisa eti mtoto amekuja wakati ambao sio wenyewe, hatuna tofauti
na Herode.
Tutetee watoto wachanga tangu akiwa
tumboni mwa mama yake, hatuwezi kusema sisi tupo huru kuangamiza maisha ya
wengine. Hakuna Mwanadamu aliyepewa uhuru wa namna hii. Ni Mungu mwenyewe
mwenye kuleta uhai na mwenye mamlaka ya kuuchukua. Kama tumefanya hivi tuache
na kumrudia Mungu.
Pia tusi waangamize wenzetu kwa hofu ya
kuogopa kupoteza umaarufu wetu. Tusiogope kujiunga nao watufundishe. Tukiwa
katika nia hii, tuenende katika nuru yake na tuziungame na kuzisafisha dhambi
zetu kwa damu yake, kama tunavyoambiwa katika somo la kwanza.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment