MASOMO YA MISA DESEMBA 28, 2020
SIKUKUU YA WAT. WATOTO MASHAHIDI
1Yoh. 1:5:2:2
Hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na
kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake.
Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo,
wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika
nuru twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Mwana wake, yatusafisha
dhambi yote.
Tukisema kwamba hatuna dhambi,
twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukizidi ungama dhambi zetu,
Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na
udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo
wala neno lake halimo mwetu.
Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili
kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba,
Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa
dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 124:1-4, 7-8
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege, katika
mtego wa wawindaji.
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia. (K)
Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu;
Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu. (K)
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu nan chi. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa
Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 2:13-18
Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama,
malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto
na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode
anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake
usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno
lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita
mwanangu.
Ndipo Herode, alipoona ya kuwa
amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto
wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye
miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliohakikisha kwa wale mamajusi.
Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa
Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali
kufarijiwa, kwa kuwa hawako.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment