ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Desemba 18, 2020.
------------------------------------------------
IJUMAA, JUMA LA 3 MAJILIO
Somo la 1: Yer 23: 5-8 Yeremia anatabiri kwamba
Bwana “atachipusha shina lenye haki kwa Daudi; kama Mfalme atatawala kwa
hekima.”.
Wimbo wa katikati Zab 72: 1-2, 12-13,
18-19 katika siku zake itachanua na haki mpaka mwezi ukome. Atakuwa na huruma
kwa wanyonge na kuwaokoa maskini.
Injili: Mt 1: 18-24 Malaika wa Mungu
alimtokea Yosefu katika ndoto na kumwambia kwamba, Mimba aliyo nayo Maria ni
kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Na kwamba ataitwa “Emanuel, yaani Mungu pamoja
nasi”
------------------------------------------------
MUNGU ANANYOOSHA MISTARI ILIYOPINDISHWA
Karibuni ndugu kwa adhimisho la Misa
Takatifu asubuhi ya leo. Wavumilivu ndio wanaomkaribisha Bwana.
Injili ya leo inatuambia jinsi kuzaliwa
kwa Yesu kulivyokuwa-kuzaliwa huku kulisaidiwa na kitendo cha wazazi wake kuwa wasikivu
na wavumilivu. Uvumilivu na usikivu ulianzia kwa Maria aliyekubali kuchukua
mimba bila ya kuwa na mume hali akijua kwamba suala hili lingalimsababishia
hatari kubwa kwa jamii yake, familia yake na hata uhai wake na maisha yake ya
baadaye.
Usikivu na uvumilivu mwingine ulitoka kwa
Yosefu aliyekubali kusikia sauti ya malaika na kumpokea Maria bila ya kujali
jamaa yake itakavyomuona kwa yeye kukubali kukiuka mila za jamii yake-kwani
kitendo cha Yosefu kumpokea Mariamu akiwa na mimba-kilimuweka hatiani,
kilimfanya aonekane kama asiye na subira. Lakini uvumilivu wake na usikivu wake
ulituletea ukombozi.
Sisi tujifunze kujitoa sadaka kwa ajili ya
wenzetu. Ni kwa njia ya kupigika kwetu wenzetu wanaweza kupona. Tusipopigika na
kusubiri wengine wapigike kwa ajili yetu, hakika tutaishia katika kilio kila
siku. Baba lazima akubali kupigika kwa ajili ya watoto wake wapate maisha bora.
Akiwa mvivu, hakuna hata mtoto wake atakayefurahia baadaye. Hata
madaktari-wasipopigika na kukesha usiku mzima wakisoma na kufanya research,
magonjwa yataizidia dunia. Kwa kupigika kwao, sisi tunapona. Kwa polisi wetu
kupigika na baridi usiku au matrafiki kupigwa jua mchana barabarani ndio sisi
tunafurahia usalama. Tukubali kupigika. Tusitegemee kila siku kula kwa wengine.
Somo la kwanza nabii Yeremia anatoa
matumaini kwamba siku zitakuja atakapochipusha toka katika shina la Daudi tawi
litakalouletea ulimwengu haki. Siku zake Yuda atafurahi. Viongozi wengi wa Yuda
walishindwa kuuletea ulimwengu furaha hii kwa sababu ya kushindwa kujitoa
sadaka kwa ajili ya wengine, wakaishia kupiga dili, kuwa mabwana na dunia
ikashindwa kupona. Sisi tuepuke kuwa mabwana, tupigike kwa ajili ya wengine.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment