Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 18, 2020

 

MASOMO YA MISA, DESEMBA 18, 2020

IJUMAA, JUMA LA 3 LA MAJILIO

 

SOMO 1

Yer. 23:5-8

 

Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.

Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri; lakini, Aishivyo Bwana, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 72:1-2, 12-13, 18-19 (K) 7

 

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani milele.

 

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,

Na mwana wa mfalme haki yako.

Atawaamua watu wako kwa haki,

Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)

 

Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,

Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.

Atamhurumia aliye dhaifu na masikini,

Na nafasi za wahitaji ataziokoa. (K)

 

Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli,

Atendaye miujiza yeye peke yake;

Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;

Dunia yote na ijae utukufu wake.

Amina na amina. (K)

 

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,

Ee kiongozi wa nyumba wa Israeli, uliyempa Musa amri zako juu ya mlima Sinai, uje kutuokoa kwa mkono wako.

Aleluya.

 

INJILI

Mt. 1:18:24

 

Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.

Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.

Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.

Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

 

 

-------------------------

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment