MASOMO YA MISA, DISEMBA 17, 2020
ALHAMISI, JUMA LA 3 LA MAJILIO
SOMO 1
MWA. 49:2, 8 – 10
SIKU ILE, Yakobo aliwaita wanawe,
akawaambia: Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, msikilizeni Israeli, baba
yenu.
Yuda, ndugu zako watakusifu, mkono wako
utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni
mwanasimba, kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; aliinama akajilaza kama
simba, na kama simba, na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi
haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sharia kati ya miguu yake, hata
atakapokuja yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1 – 4, 7 – 8, 17 (K) 7
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki
atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)
Milima itawazalia watu Amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye
kuonea. (K)
Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)
Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)
Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na
wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Hekima ya Aliye juu, unayepanga yote
kwa nguvu zako na utaratibu mwema, uje kutufunza njia ya busara.
Aleluya.
INJILI
Mt. 1:1 – 17
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa
Daudi, mwana wa Ibrahimu.
Ibrahimu akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda
akamzaa Peresi na zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu;
Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni;
Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa
Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi.
Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa
Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;
Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia
akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa
Manase; Manase akamaza Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na
ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.
Na baada ya ule uhamisho wa Babeli,
Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa
Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa
Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari;
eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo.
Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu
aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.
Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata
Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni
vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi
kumi na vinne.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment