“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Alhamisi,
Desemba 17, 2020,
Juma
la 3 la Majilio
Mwa
49: 2, 8-10;
Zab
71: 1-4, 7-8, 17;
Mt
1: 1-17
JE,
UNATAMBUA MPANGO WA MUNGU JUU YAKO?
Karibuni
ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la
Misa Takatifu. Leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na zaburi
yenye kutabiri utawala wa Masiha. Utawala huu unaelezewa kama utawala wa
kutamaniwa na wanaitamani ile haki itakayopatikana ndani yake. Maskini na
wanaoonewa wanategemewa kufurahia zaidi. Katika viongozi wote wa Israeli, hakuna
mahali popote ambapo palitokea utimilifu wa utawala huu.
Masiha
tu ndiye tumtegemeaye afanye ukamilifu wa utawala huu. Somo la Injili
linamuonesha Masiha, yaani Yesu Kristo alitoka katika uzao wa Abrahamu. Sisi
wakristo ni wazao wapya wa Abrahamu. Tulipatiwa hadhi hii kuu na Yesu. Hivyo
tutambue hadhi yetu. Tujaribu kuuiga utawala wa Yesu.
Kama
utawala huu ulivyotamaniwa kwa hamu, sisi tuishi tunu za utawala huu hasa wale
tulio viongozi. Tuwahudumie vizuri wale tunaowaongoza, wajisikie nyumbani,
wakituambia shida zao tuwajibu, tuwatie moyo, tusiwajibu kwa kashfa. Kwenye
kutoa hukumu tuhakikishe tunabakia upande wa haki, tusijiunge na wenye fedha
kukakandamiza wanyonge au kuwatelekeza. Wao wapewe nafasi ya pekee kabisa.
Katika
somo la kwanza, inadhihirishwa kwamba kabila la Yuda ambalo ndilo lililomtoa
Masiha lilipatiwa baraka maalum na Baba yao yaani Yakobo. Sisi tutambue kwamba
tabia njema na baraka tuzipokeazo duniani ni za muhimu sana. Hizi zitabariki
hata uzao wetu kwa siku zijazo. Tujitahidi pia kuwa na tabia njema na kujitunza
katika tabia hizi njema. Wengi wetu tunapoteza mengi kwa sababu ya kutojitunza,
Mama Maria aliweza kuubariki ulimwengu kwa sababu ya kujitunza. Sisi tusiache
kujitunza naye Bwana atatubariki. Tusiwe watu wa kukusanya laana toka kwa
wenzetu tunaoishi nao hapa duniani. Tuwahudumie wenzetu nasi tutajikuanyia
baraka. Tumsifu Yesu Kristo.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment