MASOMO YA MISA, DISEMBA 16, 2020
JUMATANO, JUMA LA 3 LA MAJILIO
SOMO 1
Isa. 45:6 – 8; 18:21 – 25
Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Mimi
naiumba nuru, na kuihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi
ni Bwana, niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na
yammwage haki; nchi na ifunuke ili kutoa wokovu, nayo itoe haki ikamee pamoja;
Mimi, Bwana, nimeiumba.
Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi;
Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara;
hakuiumba ukiwa, aliumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana
mwingine.
Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya
mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni
mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana
mwingine.
Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili
limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu
kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia. Kwa Bwana, peke yake
iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye na wote waliomkasirikia
watatahayarika. Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:8a, 9 – 13 (K) Isa. 45:8
(K) Dondokeni enyi mbingu, toka juu,
mawingu na yamwage haki.
Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)
SHANGILIO
Isa. 40:9 – 10
Aleluya, aleluya,
Paza sauti kwa nguvu, Wewe uhubiriye
habari njema; Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.
Aleluya.
INJILI
Lk. 7:19 – 23
Siku ile, Yohane aliwaita wawili katika
wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu, akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au
tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohane Mbatizaji ametutuma
kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa
yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo
alipojibu, akawaambia, kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea,
wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini
wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu yeyote asiyechukizwa nami.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment