MASOMO YA MISA DESEMBA 31, 2020
ALHAMISI, OKTAVA YA NOELI
SOMO 1
1Yoh. 2:18-21
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile
mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi
wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka
kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa
pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote wa kwetu. Nanyi
mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi
kwa sababu hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana
uongo wowote utokao katika hiyo kweli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1-2, 11-13 (K) 11a
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. (K)
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote
vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa
furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
SHANGILIO
Ebr. 1:1-2
Aleluya, aleluya!
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi
na kwa namna ningi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, siku hizi zilizo za
mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.
INJILI
Yn. 1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno
alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote
kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya
watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu,
jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote
wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile
nuru.
Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila
mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu
ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake
hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu,
ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi
ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema,
Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele
yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote
tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa;
neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu
wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye
aliyemfunua.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment