“ASALI ITOKAYO MWABANI”
Desemba
31, 2020.
------------------------------------------------
ALHAMISI
OKTAVA YA NOELI
Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa
Takatifu asubuni ya leo. Fumbo la umwilisho linaloelezewa na injili ya leo la
Neno aliye Mungu kutwaa ubinadamu lilileta ugumu katika kulielewa na kuliamini.
Baadhi hawakulipokea bali walitunga maelezo tofauti kulielezea na hivyo
palitokea manabii wa uongo. Baadhi yao walikuwa ni Wadoketi (Docetists)
waliosisitiza kwamba Yesu alifanania kama binadamu tu lakini kwa undani, hakuwa
binadamu. Wengine walikataa Umungu wa Yesu kabisa. Kuendana na 1 Yoh 4:1-3,
hawa kwa ujumla hawakuamini Yesu Kristo kuwa mwana wa Mungu na kwamba alikuja
kwa njia ya mwili. Ila kwa sababu Mtume Yohane aliishi kwa muda mrefu, ilimbidi
apinge uzushi wa manabii hawa kama anavyofanya katika somo la kwanza.
Nyakati zetu pia zimezidi kwa manabii wa
uongo. Wengine wanamuona Yesu kuwa kama ATM, wengine kama mtoa raha tu, wengine
hawamkubali kama Mungu. Huu ni mwaliko kwetu kwamba lazima tukatae aina hizi za
upotoshaji na kumhubiri Kristo sawasawa.
Yohane katika somo la kwanza anaendelea
kuzungumzia juu ya ujio wa manabii wa uongo. Anasema kwamba mwanzoni walikuwa
wakristo miongoni mwa jamii ya waamini lakini wakaamua kwenda kivyao. Nabii wa
uongo ni wa kuogopwa kwani hupotosha jamii yote ya waamini kirahisi kwani ni
kama mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo. Siku hizi wengi wamekwishapotoshwa na
manabii hawa.
Sisi basi habari hizi tumezisikia lakini
ni huzuni sana kwani manabii wa uongo wamekuwa wakiibuka kila siku na wamekuwa
wakipata wafuasi kila kukicha. Sisi tuombe kuwatambua manabii hawa wa uongo na
kuwapinga. Tuepuke pia kishawishi cha kujitenga na jamii ya waamini. Hiki ni
chanzo kikuu cha manabii wa uongo. Ndani ya kanisa tutashinda, nje ya kanisa
hatuwezi chochote.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment