MASOMO YA MISA, DESEMBA 27,2020
DOMINIKA, SIKUKUU YA FAMILIA TAKATIFU
SOMO 1
Ybs: 3:2-6,12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana ,
na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake
atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake, huweka akiba iliyo
azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya
kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake;
akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye.Mwanangu , umsaidie baba yako katika
uzee wake ; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake.Akiwa
amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima
sana; kwa maana sadaka apewayo baba haitasahaulika, na badala ya dhambi
itahesabiwa kwa kukudhibitisha.
Neno la Bwana……………..Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 128:1-5
Heri kila mtu amchaye BWANA,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye
katika njia zake
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako.
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye
katika njia zake
Tazama, atabarikiwa hivyo,
yule amchaye BWANA.
BWANA akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu
siku zote za maisha yako;
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye
katika njia zake.
SOMO 2
Kol.3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa
Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu,
upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya
kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya
hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue
mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa
shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote,
mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku
mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Ninyi wake, watiini waume zenu, kama
ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu
nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili
lapendeza katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije
wakakata tamaa.
Neno la Bwana …tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Kol.3:15, 16
Aleluya ,aleluya
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani
yenu
Aleluya
INJILI
Lk. 2: 22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama
ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa
katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale
Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha
Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye
alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona
Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi
walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa,
Bwana, wamruhusu mtumishi wako,Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu
yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa
mwangaza wa Mataifa,Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye
walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki,
akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka
wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga
utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii
mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa
miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni
mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na
mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na
wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana,
walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka
nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Neno la Bwana……………………sifa kwako Ee Kristo
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment