MASOMO YA MISA, DESEMBA 22, 2020
JUMANNE, JUMA LA 4 LA MAJILIO
SOMO 1
1 Sam. 1:24 – 28
Siku zile, hana alimchukua Samweli pamoja
naye, na ng’ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta
nyumbani kwa Bwana, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao
wakamchinja huyo ng’ombe, wakamleta mtoto kwa Eli.
Hana akasema, Ee Bwana wangu, kama
iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu
nawe hapa, nikimwomba Bwana. Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua
yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati
wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
1 Sam. 2:1, 4 – 8 (K) 1
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana Mwokozi
wangu.
Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana.
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui
zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako. (K)
Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata
chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto
saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.
(K)
Bwana huua, naye hufanya watu hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufurahisha mtu, naye hutajirisha;
Hushuhsa chini, tena huinua juu. (K)
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Mfalme wa mataifa na jiwe la msingi wa
Kanisa uje kumwokoa mwanadamu aliyemuumba kwa udongo.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:46 – 56
Sik ile Maria alisema: Moyo wangu
wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa
ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote
wataniita mbarikiwa; kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni
takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha. Amefanya
nguvu kwa mkono wake; amewatawanya walio na kiburi katiak mawazo ya mioyo yao;
amewaangusha wakuu kati aviti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza. Wenye njaa
amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli,
mtumishi wake; ili kukumbuka rehema zake; kama alivyowaambia baba zetu,
Ibrahimu na uzao wake hata milele.
Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu
kisha akarudi kwenda nyumbani mwake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment