MASOMO YA MISA, DESEMBA 21, 2020
JUMATATU, JUMA LA 4 LA MAJILIO
SOMO 1
Wimb. 2:8 – 14
Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama,
anakuja akiruka milimani, akichachawa vilimani. Mpendwa wangu ni kama paa, au
ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, achungulia dirishani, atazama
kimiani.
Mpendwa wangu alinena, akaniambia, ondoka,
mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, maana tazama, kaskazi imepita, masika
imekwisha, imekwenda zake; maua yatokea katika nchi, wakati wa kupelea umefika,
na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, na mizabibu
inachanua inatoa harufu yake nzuri.
Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje
zako. Hua wangu, mafichoni mwa jabali, katika sitara za magenge, nitazame uso
wako, nisikie sauti yako, maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Au.
Sef. 3:14:14 – 17
Imba, ee binti Sayuni; piga kelele, ee
Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti Yerusalemu. Bwana
ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye
Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena.
Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa,
usiogope, ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako
shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo
wake. Atakufurahia kwa kuimba.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33:2 – 3, 11 – 12, 20 – 21 (K) 1, 3
(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye
haki: Mwimbieni wimbo mpya.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
(K)
Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wako,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake. (K)
Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumaini jina lake takatifu.
(K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, uliye mng’ao wa
mwanga wa milelel na jua la haki, njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika
kivuli cha mauti.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:39 – 45
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata
nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa
Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake
Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho
Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema,
Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye
mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana
wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu,
kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri
aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment