“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Desemba 21, 2020,
Juma la 4 la Majilio
Wimb 2: 8-14;
Zab 33:2-3, 11-12, 20-21;
Lk 1: 39-45.
MAISHA YETU WIMBO WA FURAHA
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno
la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi mada yetu
kuu tunayojifunza ni kwamba Yesu ni sababu ya furaha; ujio wake ni furaha. Mama
Maria anayembeba Yesu alipofika kwa Elisabeth, Elisabethi alifurahi kabisa,
matatizo yake yaliyokuwa yakimwandama kwa kuwa na mimba aliyasahau na
kushangilia. Na hata kitoto kilichokuwa ndani ya tumbo lake kilishangilia kwa
furaha.
Somo la kwanza linatumia pichaa ya mpendwa
anayetembea juu ya milima akija kutangaza furaha. Huyu mpendwa ni Yesu na leo
inadhihirika jinsi anavyokuwa sababu ya Elisabethi kufurahi. Kama alikuwa
sababu ya Elisabethi kufurahi, hakika atakuwa sababu yetu kufurahi pia, hakika
tukimuamini hatatuacha katika hali ya kukosa imani na kukata tamaa na
matumaini.
Hakika Yesu anapaswa kuwa sababu ya sisi
kufurahi, tunapaswa kuangalia ni kipi kinachotufanya Yesu asipate kuwa sababu
ya sisi kufurahi na kubakia katika huzuni. Kikubwa ni tamaa, kutokuridhika na
kile nilichonacho na kutojiamini na kile nilichopewa na Bwana.
Kutoridhika na kile tulichopewa na Bwana
kimetufanya tuwe watu wa kuwaangalia wengine tu, tukitamani vya kwao na kusahau
kukuza kipaji tulichopewa na Bwana na ndio sababu wengi wetu ni maskini. Basi
tusikubali Yesu apite kwetu kila siku na sisi kushindwa kupata furaha kama
Elisabethi-lazima tujiulize ni kitu gani hicho kinanizuia?
Maria alimpeleka Yesu kwa Elisabethi na
hapa Elisabethi alipata kufurahi. Sisi tujifunze kuwapelekea wenzetu Yesu,
yaani habari njema. Hata kama tunaoujumbe wa kuonya au kukaripia wenzetu,
lazima tujifunze namna ya kuwaeleza ili basi nao wafarijike, mara nyingi
tumetumia lugha au mazingira mabaya na ndio maana tumeishia kuwaletea wenzetu
machungu makubwa.
Sisi tuwe kama Maria, tukifika kwa wenzetu
wafurahi. Pia kipindi hiki tuwakumbuke pia mayatima, tuwapelekee Yesu,
tuwachangie kitu, ni namna ya kuwaeleza kwamba Kristo ni wetu sote; basi
tufurahi.
------------------------
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment