Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 14, 2020

 

MASOMO YA MISA, DESEMBA 14, 2020

JUMATATU, JUMA LA 3 LA MAJILIO

 

SOMO 1

 

Hes 24:2-7.15-17

 

Siku zile Balaamu aliinua macho yake akawaona Israeli, wamekaa kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu macho asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; asema, yeyey asikiaye maneno ya Mungu, yeye aonaye maono ya Mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbulia macho; mahema yako ni mazuri namna gani, ee Yakobo, maskani zako, ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, mfano wa bustani kando yam to, mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, mfano wa mierezi kando ya maji. Maji yatafurika katika ndoo zake, na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake atadhimishwa kuliko Agagi, na ufalme wake utatukuzwa.

Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, yule mtu aliyefumbwa macho asema, yeyey asikiaye maneno ya Mungu, na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeyey aonaye maono ya Mwenyezi, akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, namwona, lakini si sasa; namtazama, lakini si karibu; nyota itatokea katika Yakobo; na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 25:4 – 6, 7b – 9 (K) 4

 

(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.

 

Ee Bwana, unijulishe njia zako,

Unifundishe mapito yako,

Uniongoze katika kweli yako,

Na kunifundisha. (K)

 

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,

Maana zimekuwako tokea zamani.

Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,

Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. (K)

 

Bwana yu mwema, mwenye adili,

Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.

Wenye upole akawaongoza katika hukumu,

Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

 

SHANGILIO

Zab. 85:7

 

Aleluya, aleluya,

Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, utupe wokovu wako.

Aleluya.

 

INJILI

Mt. 21:23 – 27

 

Siku ile Yesu alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii? Yesu akajibu, akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?

Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii. Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo

-------------------------

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment