“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Desemba 14, 2020,
Juma la 3 la Majilio
Hes 24: 2-7, 15-17;
Zab 24: 4-9;
Mt 21: 23-27
JE UNAKUBALI NGUVU NA MAMLAKA YA YESU?
Injili ya leo inaelezea juu ya mafarakano
yanayo tokea kati ya Yesu na viongozi wa dini wa wakati huo, baada ya kuwatoa
wafanya biashara nje ya Hekalu (Mt 21:12-13). Mungu-Mwenyezi, katika nafsi ya
Yesu Mwanae wa tangu milele yote, alikuwa akifundisha maneno ya uzima. Aliongea
kwa nguvu na mamlaka na kila mtu alitambua hilo. Lakini Makuhani na Wakubwa
wanaonekana wakipata hasira na wivu juu yake , huku wakimuuliza amepata wapi
mamlaka? Hili swali linaonesha ni kwa jinsi ghani hawa viongozi wa dini
walivyokuwa mbali na ukweli, walikuwa kipofu kabisa. Hawakufungua moyo kupokea
ukweli na wala hawakuwa tayari kufungua moyo na kupokea ukombozi wa Mungu
katika maisha yao. Na badala yake walisongwa na ubinafsi, majivuno na wifu.
Waliogopa kama watakubali kwamba Yohane Mbatizaji na Yesu, utume wao umetoka
Mbinguni, watapoteza umaarufu wao juu ya watu na watapoteza mamlaka yao juu ya
watu.
Sisi wote tuna uongozi katika hali flani.
Hata mazungumzo kati ya watu wawili, kila mtu anamamlaka flani. Kama ulikuwa
kwenye hilo hekalu wakati Yesu anaongea, ungejibu nini au ungefanya nini? Je,
ungemkataa? Je, ungetamani kumsikiliza zaidi? Je, utakasirishwa nae au kuwa na
wivu naye? Je, utatambua nguvu yake ya Kimungu, upendo, mamlaka nakumtafuta
yeye? Sisi pia wakati mwingine katika maisha yetu, tunajidanganya na kukimbia
ukweli, tunataka tutawale kila kitu bila hata ya Kumruhusu Mungu afanye
mabadiliko katika maisha yetu. Leo, tuamue na kukubali kupokea nguvu ya Mungu
na tumruhusu yeye awe dereva wa maisha yetu katika furaha na ukamilifu wote.
Sala: Bwana, nisaidie kuisikia sauti yako
ya utakatifu kila mahali. Nisaidie niweze kukutambua wewe kila mahali
ninapoenda. Na ninapo kutafuta nisaidie nifurahi kwa kukupata wewe na kukubali
yote kwa ujasiri unayosema. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment