MASOMO YA MISA DESEMBA 13, 2020
JUMAPILI, DOMINIKA YA 3 YA MAJILIO
MWANZO:
Flp. 4:4-5
Furahini katika Bwana siku zote; tena
nasema furahini. Bwana yu karibu.
SOMO 1
Isa. 61:1-2, 10-11
Roho ya Bwana Mungu I juu yangu; kwa
sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma
ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao
waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,
na siku ya kisasi cha Mungu wetu.
Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu
itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika
vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi
arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko
yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana
Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Lk. 1:46-50, 53-54 (K) Isa. 61:10
(K) Nafsi yangu itashangilia katika Mungu
wangu.
Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi
wangu;
Kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi
wake.
kwa maana, tazama, tokea sasa
vizazi vyote wataniita mbarikiwa. (K)
kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
na jina lake ni takatifu.
Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kw ahao wanaomcha. (K)
Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake. (K)
SOMO 2
1Thes. 5:16-24
Furahini siku zote; ombeni bila kukoma;
shukuruni kw akila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo
Yesu.
Msimzimishe Roho; msitweze unabii;
jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna.
Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa;
nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama,
wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita,
naye atafanya.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 4:18
Aleluya, aleluya,
Roho wa Bwana yu juu yangu, amenituma
kuwahubiri maskini habari njema.
Aleluya.
INJILI
Yn. 1:6-8, 19-28
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu,
jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote
wapate kuamini kw ayeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile
nuru.
Na huu ndio ushuhuda wake Yohane, Wayahudi
walipotuma kwake makuhani wa Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u
nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo.
Wakamwuliza, Ni nani basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule?
Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka.
Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani,
Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.
Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa
Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza,a ikiwa wewe si
Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohane akawajibu akisema, Mimi nabatiza na
maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma
yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika
huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohane akibatiza.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment