Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA DESEMBA 12, 2020

 

MASOMO YA MISA DESEMBA 12, 2020

JUMAMOSI, JUMA LA 2 LA MAJILIO

 

SOMO 1

Ybs. 48:1-4,9-11

 

Ndipo aliposimama Nabii Eliya, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta taa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifungu mbingu, na mara tatu kutoka huko akateremsha moto. Jinsi unavyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako aona fahari.

Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli.

Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 80:1-2,14-15,17-18 (K) 3

 

(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe, Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.

 

Wewe uchungaye Israeli, usikie,

Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;

Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,

Uziamshe nguvu zako,

Uje, utuokoe. (K)

 

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,

Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.

Na mche ule ulioupanda.

Kwa mkono wako wa kuume;

Na tawi lile ulilolifanya,

Kuwa imara kwa nafsi yako. (K)

 

Mkono wako na uwe juu yake,

Mtu wa mkono wako wa kuume;

Juu ya mwanadamu uliyemfanya,

Kuwa imara kwa nafsi yako;

Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;

Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako. (K)

 

SHANGILIO

Lk. 3:4,6

 

Aleluya, aleluya,

Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,

Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,

Aleluya.

 

INJILI

Mt. 17:10-13

 

Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu wakisema: Kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?

Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote; ila nawaambia ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.

Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

 

 

-------------------------

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment