MASOMO YA MISA,
ALHAMISI, 24 DESEMBA 2020
JUMAMOSI YA 4 YA MAJILIO
SOMO 1
2Sam. 7:1-5, 8-11, 16
Ikawa, mfalme Daudi alipokuwa akikaa
katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake
waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi
ninakaa nyumba mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani
akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu
pamoja nawe.
Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana
likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana
asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Nalikutwa katika
zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya
Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui
zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko
duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate
kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa
tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru
waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui
zako wote.
Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana
atakujengea nyumba. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele
mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 89:1-4, 27, 29 (K) 1
(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa change nitavijulisha vizazi
vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu
wako. (K)
Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele;
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata
milele. (K)
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa
kwanza;
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
Wazao wake nao nitawadumisha milele,
Na kiti chake cha enzi kama siku za
mbingu. (K)
SHANGILIO
Aleuya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, Uliye mnga’ao wa
mwanga wa milele na jua la haki, Njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika
kivuli cha mauti.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:67-79
Siku ile, Zakaria, baba yake Yohane
alijazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,
Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa
amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu katika
mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo kwa kinywa cha
manabii wake watakatifu; tuokolewe na adui zetu na mikononi mwao wote
wanaotuchukia; ili kuwatendea rehema baba zetu, na kulikumbuka agano lake
takatifu; uapo aliomwambpia Ibrahimu, baba yetu, ya kwamba atatujalia sisi,
tuokoke mikononi mwa adui zetu, na kumwabudu pasipo hofu, kwa utakatifu na kwa
haki mbele zake siku zetu zote.
Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake aliye juu,
kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umemtengenezea njia zake;
uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema
za Mungu wetu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, kuwaangaza
wakaao katika giza na uvuli wa mauti, na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya
Amani.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment