ASALI
ITOKAYO MWMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Jumanne,
Novemba 24, 2020,
Juma
la 34 la Mwaka wa Kanisa
Ufu
14:14-19;
Zab
95:10-13;
Lk
21:5-11
KUJIANDAA
KWA MWISHO WA ULIMWENGU!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza na hapa tunakutana na malaika akitumwa
kutangaza ujio wa mwisho wa maisha ya dunia kwa kutumia lugha ya kuvuna mazao
ya dunia. Wanadamu wa dunia wanaonekana kuwa kama mazao ambayo mkulima
atayavuna. Nafaka njema ataikusanya ghalani, mbovu itaharibiwa.
Mfano
huu unaonyesha hali halisi ya mwanadamu; ama kweli mwanadamu anayo kila sababu
ya kuacha kujivuna, na kutulia na kujiweka zaidi mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
Tunapaswa kuwa mazao bora tukubaliwe na mkulima. Tujipalilie kwa njia ya sala,
huruma, ukarimu, upole na unyenyekvu. Tuepuke matendo yanayotufanya tukose afya
kama uzinzi, moyo usiosamehe, ulevi, maneno machafu na picha chafu. Haya
yanatudhoofisha, tunabakia na mawazo mazito, hatusongi mbele. Yanatufanya pia
tuwe maskini wa kifedha. Wengi kati yetu ni maskini kwa sababu ya kutumia pesa
kuzini ovyo na kunywa kupita kiasi. Yametukosesha na familia zetu na kuwafanya
watoto wetu wabakie bila elimu au ujuzi wa kufaa. Mwishowe yanatukosesha
mbingu. Sisi tujipalilie na tusikubali kuwa dhaifu.
Katika
injili, Yesu anaeleza kwamba nyakati za mwisho kutatokea magumu mengi
yatakayosumbua imani yetu. Ni imani iliyotulia tu ndio itakayoweza kuyashinda
magumu haya.
Hii
ni kweli ndugu zangu, bila imani tulivu na imara hatutayaweza haya magumu. Haya
magumu yanatutokea kila siku na kukumbana na vishawishi. Ukipita unakuta vibao
vinakuambia jiunge freemason, au kuna mganga anayesafisha nyota au ingia kwenye
biashara fulani haramu. Tayari walio na tamaa na uchu wa mali wameiacha imani
yao na kujaribu kujiunga hivi vikundi. Haya yote yatatokea na wengi watapotea
sana. Ni wale tu wenye imani thabiti watakaoweza kustahimili kuyashinda magumu
haya na kuruhusu wasiyumbishwe na vishawishi hivi. Sisi tuzidishe unyenyekevu
kama wanaotambua kwamba muda sio mrefu itatubidi kuvunwa kama mavuno. Tuzidishe
imani ili ajapo mvunaji atukute tukiwa na afya njema.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment