“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi,
Oktoba, 24, 2020,
Juma
la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef
4:7-16;
Zab
121:1-5;
Lk
13:1-9
THAMANI
YA WAKATI WA SASA!
Karibuni
ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa Takatifu
asubuhi ya leo. Leo basi Paulo anawaeleza Wakristo wa Efeso kwamba Kristo
aliposhuka kuzimu na baadaye kupaa, aliweza kuwakweza wanadamu ndani ya Kanisa.
Wakristo tulipata nafasi kupokea vipaji mbalimbali: wengine tukifanywa waalimu,
wengine mitume, wengine waenjili. Vyote hivi ni zawadi tosha toka kwa Mungu.
Kila mmoja alimpatia kipaji na hadhi yake, alimwimarisha ili basi asipeperushwe
tena na upepo. Hivyo tunapaswa basi kusimama imara, tujiamini; Kristo ametupatia
uwezo na hadhi kubwa na katika Lk 10:29, anasema kwamba ametupatia uwezo wa
kukanyaga nge na nyoka.
Wengi
tunashindwa na shetani kwa sababu hatujiamini. Shetani ametuonea sana,
hatuamini kwamba Kristo ametupa uwezo, hata tunapokuwa katika kuadhimisha mafumbo
matakatifu-tunasema baadhi yetu je, hivi vitu ni kweli? Tutambue kwamba
tukishindwa kujiamini, basi ndio mwanzo wa sisi kushindwa kwa mengi. Tujiamini
ndugu zangu ili tumpatie sifa na shetani asitutese tena. Shetani anatabia ya
kutufanya tusijiamini, tujisikie kwamba hatuna uwezo na hili linatufanya
tushindwe kwa mengi na kurudi nyuma. Tusikubali kurudi nyuma kila siku.
Katika
somo la injili Yesu anatoa mfano wa walioangukiwa na mnara na kufa kifo kibaya
na kufundisha kwamba haimaanishi hawa wanaopatwa na mkasa huu ndio wadhambi.
Wakati
mwingine sisi tunaobaki ndio wadhambi zaidi. Kile kipindi cha sisi tunabakia
bila kuadhibiwa na tunabakia kusikia na kuona maumivu ya wengine ni kipindi cha
kutufunza ili tuache dhambi. Ajali za wengine na mateso yao unayaona kwenye tv,
au wakimbizi wakilia yote haya ni nafasi zitutakazo tuongeze bidii tuweka
samadi ya kiroho. Ni kipindi ambacho tunatiliwa samadi kama huyu mkulima
anavyofanya kwa huu mti wake ili tubadilike na tusipobadilika tutakatwa.
Wadhambi
wengi tunaendelea kuishi kwa sababu ya huruma ya Mungu. Kati yetu tunaishi na
watu ambao labda tungaliomba wawe wamekwishaadhibiwa tayari lakini Yesu
anaruhusu waendelee kuishi ili basi wabadilike, ni huruma ya mkulima. Sisi
tubadilike na tukiona hatujaadhibiwa tusijione ati sisi ni wajanja sana au
Mungu hana nguvu. Mungu akiamua, nakueleza sisi hatutasalia. Tuombe kutumia
nafasi tupewazo vyema. Wengi tunatumia vibaya kile kipindi Mungu anapokaa kimya
na kuamua kumtukana na kumwona kana kwamba hana nguvu. Kwa hapa tunajilaani
zaidi. Mungu ni mkuu kila wakati. Tuache kumkosea adabu.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment