“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Alhamisi,
Oktoba 22, 2020,
Juma
la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef
3:14-21
Zab
32:1-2, 4-5, 11-12, 18-19
Lk
12: 49-53
MUNGU
NI MOTO UNAOPENDEZESHA VYOTE.
Ndugu
zangu katika Kristo karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asuhuhi ya leo. Leo
tuanze tafakari yetu kwa kuiangalia zaburi yetu, ambapo tunamuona Mzaburi
akituambia kwamba nchi imejaa fadhili za Bwana. Kila kitu kilichopo ulimwenguni
pamoja na uzuri wake wote ni mali ya Bwana. Hivyo hizi fadhili za Bwana
tuzitumie huku tukijua sio zetu ni za Bwana. Tuzitumie kwa ukarimu tukifahamu kila
fadhili ni mali ya Mungu. Yeye hufurahi tunaposhirikisha hizi fadhili bila
uchoyo.
Ndugu
zangu Zaburi hii inatilia mkazo ujumbe wa Paulo kwa Waefeso, anawaeleza
watambue wao wamekuwa wamoja na Mungu ni Baba yao kwa njia ya Kristo. Hivyo
wahakikishe wanatiwa nguvu kwa Roho wa Kristo wabaki katika imani moja na tena
wakiwa katika shina kuu la upendo. Paulo anamshukuru Mungu kwa zawadi hii.
Ndugu
zangu tunajifunza kitu hapa kwamba sisi Mungu ni Baba yetu zote na fadhili zote
ulimwenguni ni mali yake. Tusidhulumu wala kujivuna tuongozwe na Roho wa Kristo
tena kwa imani tukiwa tumejawa mapendo na wala tusibaguane. Tukifanya hivi kwa
kuondoa wivu, na madhulumu yote kila mtu atakiri kweli sisi ni watoto wa Mungu
kwa njia ya Kristo.
Katika
Somo la Injili Yesu anatupa tahadhari nyingine kwamba kwa ujio wake yaweza kuwa
amekuja kuwasha moto duniani. Na hili kweli linatokea nyakati zetu,
tumeshuhudia familia zikitengana kwa kigezo cha Injili tena wote wakiwa wafuasi
wa Kristo. Wengine hujidai wanamuelewa Kristo zaidi na kuwadharau wengine.
Wengine huamka hata usiku wa manane na kuwasumbua wengine kwa sala za kelele
kwa kisingizio wanafukuza pepo na kuwafanya wengine wasilale. Wengine hujifanya
wafafanuzi wazuri wa maandiko zaidi kuliko wengine na hivyo kuishia kushindana.
Yesu haya aliyatambua yatakuwepo. Paulo anatupatia jibu zuri sanaa katika somo
la kwanza, hamna namna nyingine ya kuonesha kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo
isipokuwa kwa njia ya upendo. Utengano sio sifa ya Kristo.
Tusitumie
pia sala kama kisingizio cha kuwakashifu wale wasio sali. Tusijione wema zaidi
kwasababu tu sisi tunaenda kanisani na wengine hawaendi. Badala yake sisi
tuwaombee waregevu na kuwashauri kwa upendo na upole ili waweze kuvutwa nao
kumtumikia Kristo. Tusiwashe moto duniani wa fujo kwakutumia Injili ya Kristo.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment