“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu,
Oktoba 19, 2020,
Juma
la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef
2:1-10
Zab
100:2-5
Lk
12:13-21
KUWA
TAJIRI KUMWELEKEA MUNGU!
Karibuni
ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo
tafakari yetu ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo
Paulo anawaeleza Waefeso juu ya upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo:kwamba
wamepata bahati zaidi ya wenzao. Wao wamekombolewa toka katika maisha yasiyofaa
kwa damu takatifu ya Kristo. Hivyo basi wajifunze kutambua upendo na ukuu huu
wa Kristo.
Waefeso
wanaambiwa hivi kwa sababu baadhi yao walianza kulegalega na kuanza kutamani
maisha waliyoishi wale wapagani wakifikiri kwamba wanafaidi zaidi. Hivyo
walishindwa kuona nguvu ya Kristo maishani mwao. Paulo anawaambia wamkumbatie
Kristo ili basi waweze kuiona nguvu yake maishani.
Ndugu
zangu, kilichowatokea Waefeso kinazidi kututokea na sisi kila siku. Wengi wetu
tunashindwa kuiona nguvu ya Kristo kwa sababu bado tunatabia ya kutamani maisha
mengine-tunafikiri kwamba wanaoishi maisha yasiyo na Kristo wanafaidi zaidi.
Tamaa ya namna hii imetukosesha mengi katika uhusiano wetu na Kristo. Tamaa
zinatufanya tuwe wachoyo wa kumpatia Mungu nafasi yake. Tunashindwa kutoa hata
kasehemu kadogo ya muda wetu hata kasehemu sifa yetu kwa ajili ya Kristo. Sisi
tuzidi kumkumbatia Kristo naye atatuonyesha nguvu zake maishani mwetu zaidi na
zaidi.
Mfano
mzuri wa tamaa tunakutana nao leo katika injili yetu. Tajiri huyu alizidisha
tamaa-akawa mchoyo wa kumpatia Mungu hata kasehemu cha sifa kwa kumwezesha
kufanikisha mazao mengi hivyo. Kama angalimpatia Mungu nafasi yake,
asingalikuwa na cha kupoteza lakini tamaa zilimfanya aone shida hata kuzungumza
neno moja amshukuru Mungu. Hii iliyomtokea huyu tajiri inatutokea na sisi kila
siku. Sisi tunapoteza mengi kwa sababu ya kuona ugumu kutumia hata dakika tano
kumshukuru Mungu-yaani dakika tano tu. Sio zaidi. Tunapewa masaa yote 24 kwa
ajili ya shughuli zetu tu lakini dakika tano za kumrudishia Mungu tunaona
shida.
Tunaishia
hata kukosa kanisani jumapili ili tuzalishe mali. Hii sio sahihi. Lazima
tubadilike ndugu zangu. Wengi wetu ni maskini na tumenyanganywa mengi kwa
sababu ya kukosa kuwa na shukrani tu. Ndio hiyo tu. Tunapata milioni moja
lakini tunaona ugumu kutoa hata shilingi elfu kumi umpatie Mungu shukrani.
Jamani! Hapa hatujafanana na huyu tajiri? Tunapokea mshahara wa laki nne lakini
maskini akija akiomba hata hapo miatano tunakataa. Tubadiilike yasije
yakatutokea yaliyomtokea huyu tajiri.
Tunashuhudia
watu wakikazana kutafuta mali kila siku asubuhi na mchana ili wawe nazo lakini
wanaondoka na kuziacha bila ya wao kutumia kitu chochote-au wanaziacha kwa
watoto wao ambao huzitapanya na kuishia hivihivi tu. Au zile mali zinakuja
kupotea potea na kutumiwa hata na watu ambao hata hapo mwanzo hawakuzifanyia
kazi. Matukio yote haya yatufanye tubadilike.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment