Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 11, 2023


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 11, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 31 LA MWAKA
Kumbukumbu ya Mt. Martini wa Tours
_____________
SOMO 1
Rum. 16:3-9, 16, 22-27

Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.

Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo. Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu. Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana. Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu. Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo wawasalimu.

Mimi Tertio, niliyandika waraka huu, nawasalimu katika Bwana. Gayo, mwenyeji wangu na wa Kanisa lote pia awasalimu. Erasto, wakili wa mji, awasalimu, na Kwarto, ndugu yetu.

Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo na ile amri iliyositirika tangu zamani za milele, ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii ikajulikana na mataifa yote kama alivyowaamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani. Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kriso, milele na milele. Amina.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
_____________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:2-5, 10-11

(K) Nitalihimidi jina lako milele, Ee Bwana.

Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.

Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yake,
Kitayatangaza matendo yake makuu.
Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
Na matendo yako yote ya ajabu.

Ee Bwana, kazi zako zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
_____________
SHANGILIO
Yn. 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
_____________
INJILI
Lk. 16:9-15

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Bali, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu au kumpenda huyu, ama atamshikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
_____________

Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment