“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Julai 24, 2024.
JUMA LA 16 LA MWAKA
Kut 16:1-5, 9-15;
Zab 78:18-19, 23-28;
Mt 13:1-9.
MBEGU NENO LA MUNGU!
Yesu amekuja kutoka mbingu za juu kabisa za hekima na utukufu kuja kuwafundisha wavuvi, wakulima, watoza ushuru na hata akina mama wa nyumbani. Alitumia mifano ya kawaida ili aweze kuwafunulia mafumbo ya Mbinguni ili waweze kuelewa. Leo katika Injili akiwa kwenye mashua anawahutubia makutano juu ya mfano wa mpanzi. Yesu anatumia akili ambazo wanazo ili kuweza kuwaelezea akili ile ambayo hawana, anatumia vitu vya kawaida vya ulimwengu ili kuelewa vile vya juu wasivyo vielewa. Kutoka mambo ya kushikika mpaka mambo ya kiroho. Kutoka utawala wa binadamu mpaka utawala wa Mbinguni.
Mbegu ni neno la Mungu na shamba ni mioyo ya watu. Swali ni kwamba tupo tayari kulipokea neno lake na kuliruhusu lipenye ndani ya mioyo yetu na kuzaa matunda? Ni katika utulivu na kulisikiliza neno lake tuu tunaweza kufahamu mapenzi yake. Mioyo yetu inapaswa kuwa kama ule udongo mzuri. Udongo mzuri katika mioyo yetu sio rahisi kuupata, ni rahisi zaidi kuwa udongo uliokauka, wenye miiba, miamba. Lakini ukweli ni kwamba udongo wenye rutuba unahitaji majitoleo na muda. Kitu cha muhimu kabisa ni kukimbilia unyenyenyekevu wa kweli. Ukweli wa kukubali kwamba sisi hatuna nguvu yeyote bila neema ya Mungu ni mwanzo mzuri wa kukubali mioyo yetu kupata udongo mzuri. Kuanzia pale tunapaswa kumwamini Mungu asilimia zote. Tukiwa wanyoofu na kujikabidhi kwake tutakuwa tayari kumsikiliza anapo ongea.
Atakapo ongea tutasikiliza na kumtii kwa furaha. Ni kwa njia hiyo matunda mazuri ya huruma yake yanaweza kuzalishwa katika mioyo yetu na kwenda katika maisha ya wengine. Daima tafuta kutengeneza udongo mzuri katika mioyo yetu na Mungu atatusaidia kuzaa matunda.
Sala: Bwana nisaidie mimi niweze kuwa udongo mzuri wa neno lako. Ninakuomba nisikilize yote unayoniambia ili niweze kupanda mbegu ya imani ndani mwangu. Ninakuomba Imani hii ikuwe na kuleta Baraka unazotaka. Yesu nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment