MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2024
JUMATANO, JUMA LA 16 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Yer. 2:1, 4 – 10
Maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani
waliokuwa katika Anathothi, katika nchi ya Benyamini.
Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika
tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii
wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana Mungu, tazama, siwezi kusema; maana
mimi ni mtoto.
Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana
utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno
nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao; maana mimi nipo pamoja nawe
nikuokoe, asema Bwana.
Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa
changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia,
nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na
kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 71:1 – 6, 15, 17 (K) 15
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe. (K)
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda siku zote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uiopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)
Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima. (K)
Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.
Mchana kutwa; maana sijua hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:1 – 9
Yesu alitoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.
Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano
wote wakasimama pwani.
Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama,
mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine
zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye
miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na
jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine
zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye
udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye masikio
na asikie.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment