“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumapili, Juni 5, 2022.
Dominika ya
Pentekoste
Sherehe ya Pentekoste
Mdo 2: 1-11;
Zab, 104: 1, 24, 29-31,
34;
1 Kor 12:3-7, 12-13 au
Rom 8:8-17
Yn 20:19-23 au Yn
14:15-16, 23-26
WEKA ULIMWENGU KWENYE
MOTO WA MAPENDO YA MUNGU
‘Pentekoste’ ni neno la
Kigiriki lenye maana ya “Hamsini”. Wakristo wanasherekea sherehe hii siku
hamsini baada ya Pasaka (Mdo 2). Ikiwa ni tamaduni iliyotoka Agano la Kale,
yenye maana ya “sikukuu ya mavuno” katika siku ya hamsini baada ya “Pasaka ya
Wayahudi” (Kut. 23:16, Hes. 28:26-31, Kum. 16:19-21). Siku hii ilikuja kuwa
muhimu kwa Wakristo kwasababu, majuma saba baada ya ufufuko wa Yesu, wakati wa
sikukuu ya mavuno ya Wayahudi, Roho Mtakatifu aliwashukia wafuasi wa kwanza wa
Yesu, akiwapa nguvu na uwezo wakumtangaza Kristo na kuwakusanya pamoja kama
Kanisa. Kama Wayahudi walivyokuwa wakitoa matunda ya mazao yao ya kwanza,
wakijiandaa kwa mvua kwa ajili ya mazao yajayo; wafuasi, mazao ya kwanza ya
utume wa Kristo yaliyoiva, wanapokea mvua ya Roho Mtakatifu, Roho atakaye
wafanya wakue na kuwa mazao na mbegu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Katika Siku
hii, umoja wa watu wa Mungu kama Kanisa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ulianza.
Roho Mtakatifu alitumwa
kama Yesu alivyo ahidi, ili kukamilisha kilele cha ufunuo wa upendo wa Mungu.
Roho Mtakatifu hajiweki kwa Wayahudi peke yao, bali anafunua upendo wa Mungu
usio na mipaka kwa watu wote, akileta Baraka, matunda katika nchi ambayo
ilikuwa imelaaniwa kipindi cha Adamu na Eva. Lugha iliyoleta mtafaruku
nakutoelewana katika mnara wa Babeli, inakuwa kiunganisho kikuu kwa njia ya
Roho Mtakatifu. Ukosefu wa urafiki na umoja na Mungu uliopotea katika Edeni,
Roho Mtakatifu anaurudisha tena kwa kuwa na Kanisa daima.
Pentekoste
tunasheherekea kazi na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu kama waumini na
Kanisa. Mungu amemimina juu yenu wote Roho Mtakatifu (Rom 8:1-11) na tunapaswa
kuishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu anatusaidia
kumkiri Yesu kwamba ni Bwana wetu (1 Kor 12:3), akituwezesha kumtumikia Mungu
(1 Kor 12:4-11), akituunganisha pamoja kama Mwili wa Kristu (1 Kor 12:12-13),
anatusaidia kusali (Rom 8:26), anatuombea ndani ya Mungu Baba (Rom 8:27). Roho
Mtakatifu anatuongoza (Gal 5:25) na Roho Mtakatifu anatusaidia tuishi kama Yesu
(Gal 5:22-23).
Baba Mtakatifu Fransisko
anamuita Roho Mtakatifu “Upendo” unaokosekana ndani ya familia zetu na
Ulimwenguni. Katika ujumbe wake wa siku hizi tuu ndani ya “Amoris Laetitia”,
“Furaha ya Upendo” anamuonesha Roho Mtakatifu kama mfano halisi wa Familia za
Kikristo na Kanisa. “Upendo ndani ya familia
ya Kimungu, ni Roho Mtakatifu….tunaweza kutambua upendo wa Mungu ndani ya Roho
Mtakatifu….kwa njia ya Kanisa, ndoa na familia zinapokea neema za Roho
Mtakatifu kutoka kwa Kristo, ili tuweze kutoa ushuhuda wa Injili ya Upendo wa
Mungu.” Baba Mtakatifu
anazialika familia zote za Kikristo “kila wakati kualika usaidizi wa Roho
Mtakatifu anayetakatifuza umoja wenu, ili neema zake ziweze kutawala katika
kila jambo mnalokutana nalo”. Pia anasema, bila Roho Mtakatifu umoja wa familia
za Kikristo hauwezekani. “hakuna hata moja kati ya haya, litakalo wezekana bila
kusali kwa Roho Mtakatifu ili amimine neema zake, nguvu zake na moto wa Roho,
kutufanya wake, kutuongoza na kubadili mapendo yetu kwa kila hali”
Leo tunaitwa, tuweze
kujali kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu binafsi, familia, jumuiya na
Kanisa zima. Je sisi ni vyombo vya kazi ya Roho Mtakatifu? Je, tumekuwa
wasikivu wakati Roho Mtakatifu anapotuongoza? Matunda ya Roho Mtakatifu
(Upendo, furaha, Amani nk.) yanakuwa ndani mwangu? Sisi wote tunaishi ndani ya
uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu lakini katika viwango tofauti. Tunazuiwa na
uoga wetu, dhambi zetu, Mapungufu yetu na uharibifu wetu wa kila siku
unaotufanya tushindwe kuhisi uwepo wa zawadi ya Mungu ya Upendo ‘Roho
Mtakatifu’. Pentekoste inatupa tena wakati wa kuhisi moto wa Roho Mtakatifu na
kuuweka Ulimwengu kwenye moto wa upendo wa Mungu.
Sala: Nivuvie nguvu ya
Roho Mtakatifu Bwana, ili mawazo yangu yaweze kuwa matakatifu. Nivuvie pia
nguvu ya Roho Mtakatifu ili kazi yangu iweze kuwa takatifu. Gusa moyo wangu
Roho Mtakatifu, niweze kupenda vile vitakatifu tu. Nipe ujasiri Roho Mtakatifu
ili niweze kulinda kila kilicho kitakatifu. Nilinde Roho Mtakatifu, ili niweze
kuwa Mtakatifu daima. Roho Mtakatifu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment