MASOMO YA MISA, JUNI 5, 2012
SHEREHE YA PENTEKOSTE
SOMO 1
Mdo. 2:1-11
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako
wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa
nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi
zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote
wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho
alivyowajalia kutamka.
Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu
watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa
makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia
wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana,
Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu
lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao
Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na
pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya
Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATI KATI
Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30
(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya
upya uso wa nchi. au: Aleluya.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)
Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)
SOMO 2
1 Kor. 12 :3-7, 12-13
Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa
katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za
kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini
kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo
vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo
hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili
mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu
huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini
wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.
INJILI
Yn. 20 :19-23
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale
walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu,
akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo,
akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi
walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama
Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo,
akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi,
wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment