Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 10, 2024


MASOMO YA MISA, JUNI 10, 2024
JUMATATU, JUMA LA 10 LA MWAKA


SOMO 1 
1 Fal. 17 :1-6

Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.

Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 121:1-8 (K) 2

(K) Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi.

Nitayainua macho yangu niitazamc milima;
Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. (K)

Asiuache mguu wako usogezwe;
Asisinzie akulindaye;
Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi,
Yeye aliye mlinzi wa Israeli. (K)

Bwana ndiye mlinzi wako;
Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. (K)

Bwana atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa na hata milele. (K)


SHANGILIO 
Zab. 119:34

Aleluya, aleluya, Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, nitaitii kwa moyo wangu wote. Aleluya.


INJILI
Mt 5:1-12

Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, 

Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.
Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.


Copyright © 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment