“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Juni 11, 2023
Juma la 11 la Mwaka wa Kanisa
Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu (Corpus Christi)
Kumb 8: 2-3, 14-16;
Zab 147;
1 Kor 10: 16-17;
Yn 6: 51-58.
EKARISTI-UJUMBE MKUBWA WA UPENDO WA NYAKATI ZOTE.
Sister Muagustiniani, sister Juliana wa Liège (Belgium) alipata maono ya
kanisa likiwa chini ya mwezi unaongaa wenye kidoti kimoja cheusi. Doti hii
ikionesha kutokuwepo kwa sherehe ya Ekaristi. Hii ilifanya baadaye kuwepo na
sherehe ya Mwil na Damu ya Kristo ambayo iliwekwa kwenye kalenda ya Litirujia
ya Kanisa mwaka 1264 chini ya Papa Urban wa IV. Je kulikuwa na haja ya kuwa na
sherehe hii ya Ekaristi? Sherehe kama hii kawaida inatupa nafasi ya pekee ya kumshukuru
Mungu kwa zawadi ya uwepo wa Kristo kuwa nasi daima, ambaye yupo kweli katika
Ekaristi Takatifu. Kwa upande mwingine, ni wakati wetu wakutafakari fumbo hili
kubwa la upendo. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ambayo ni kilele cha
Sakramenti zote, ndani yake Sakramenti nyingine zote huadhimishwa, kwasababu ni
“Fumbo la mafumbo yote” na “Taji la Sakrament zote” sakramenti zote zinavishwa
taji na Ekaristi Takatifu. Katika Ekaristi Takatifu hatupokei tuu neema bali
tunampokea Bwana wa Neema.
Ekaristi Takatifu ni kilele cha sala sote na kuabudu kwetu. Hakuna njia
nyingine ya kuwasiliana na Mungu, yenye undani na ukuu zaidi ya Ekaristi
Takatifu. Hapa watu wawili (mtoaji na mpokeaji) wanakuwa katika umoja wa kweli,
(ndani yake, naye ndani mwako). Tunapaswa kusali mara nyingi katika hali zote
na sehemu yeyote kwasababu sala hizi zinatufanya tuunganike na Bwana na kujenga
umoja naye. Lakini kwakweli, hakuna sala yeyote inayotoa muunganiko mkuu zaidi
ya Ekaristi Takatifu. Hakuna yeyote wala chochote kinachopaswa kutufanya
tushindwe kuwa wamoja na Kristo, na kwa njia ya umoja huu tupate nguvu
tunayohitaji katika maisha yetu.
Jumapili hii tumekuja pamoja kuadhimisha Ekaristi Takatifu kwa roho ya
furaha na mapendo. Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya Wakatoliki wengi ambao
hawaioni Ekaristi Takatifu katika hali tena. Idadi ya Wakatoliki wanao shiriki
adhimisho la Ekaristi jumapili, baadhi ya sehemu inashuka kila mara. Misa sio
sehemu ya maonesho, hawapati kile wanachotaka, watu wanapenda kitu kipya kila
wakati na tena pengine chenye mtizamo wanaotaka wao. Ni ajabu utakuta Misa
zinazo hudhuriwa mara nyingi ni, Jumatano ya Majivu, Jumapili ya Matawi,
Jumapili ya pasaka na Noeli kwasababu kuna vitu ninaongezwa ndani yake kwa
mfano, matawi, majivu, mishumaa nk. Wengi wanategemea Padre aweke utani kwenye
mahubiri ili afanye watu wachangamke, wengine wanataka kwaya waimbe vizuri sana
kwa sauti zenye kupendeza na pengine wacheze sana kwa midundo ya kisasa zaidi,
vifaa bora zaidi vya muziki, wengine wanataka wasomaji wenye sauti nzuri
zakupendeza masikioni mwao, viti vizuri vya kukaa, taa zenye mwanga mzuri wa
kupendeza na vifaa vizuri vya sauti. Kwa kweli, haya yote ni mitazamo na
matarajio. Mbaya zaidi, pengine wapo pia baadhi ya makuhani wamenaswa kwenye
mtego huu. Badala ya kuwapa watu anachosema Mungu, anawapa watu wanachopenda
kusikia na kuona. Kwa matokeo haya, neno la Mungu halihubiriwi kiaminifu na
katika unabii na maana halisi ya Uwepo wa Mungu inapotezwa. Kumekuwako na ile
hali ya mlalo (mwanadamu kwa mwanadamu) na kuacha ile hali ya wima (Mungu
kwenda kwa Mwanadamu) ya liturujia.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikti XVI alikuwa akisisitiza kila wakati kwamba
“Liturjia ni Tendo la Mungu”. Hatupaswi kusahau kwamba kiini cha liturujia na
maadhimisho ya Sakramenti ni Mungu na sio mwanadamu. Aliendelea pia kusema;
“Katekesi nzuri juu ya Ekarisiti ni Ekaristi yenyewe ikiadhimishwa vizuri”.
Kufahamu na kuamini kwamba Yesu yupo kweli katika adhimisho la Ekaristi,
tunapaswa wote tufanye jitihada kufanya adhimisho hili lenye maana na furaha.
Bila kusahau kwamba Ekaristi haiwi Ekaristi kwasababu ya Imani ya padre au
Muumini. Baada ya sala ya Ekaristi (Konsekratsio) Yesu anakuwa kweli chini ya
Maumbo ya mkate na divai. Uwe na Imani au usiwe na Imani, Yesu anabaki kuwa
Yesu katika maumbo hayo daima. Tunadaiwa kuwa na Imani ili tuweze kushirikiana
na neema ya Mungu lakini hata tusipokuwa nayo haimaanishi utamzuia Yesu kuwa
katika maumbo hayo. Tushirikiane naye kwa Imani ili tupate neema.
Ni Mtakatifu Maximiliani Kolbe ambaye aliwahi kusema kwa hakika kwamba,
“Utimilifu wa Misa sio wakati wa mageuzo bali ule umoja mtu anaoupokea wakati
wa komunyo”. Tunaamini kwamba Ekaristi ni sadaka ile ile aliyo itoa Yesu pale
msalabani na sio kumbukumbu ya kihistoria ya tukio lililopita, na kwamba mkate
na divai unakuwa kweli mwili na damu ya Kristo, na pia tunaamini kwamba
Ekaristi ni sakramenti ya Upendo wa Mungu kwetu. Sakramenti inayo adhimishwa
katika Imani hiyo inatusaidia tuweze kuuona umoja wa ndani wa mtu na Mungu.
“Wakati tunatazama Msalaba, unatambua ni kwajinsi ghani Yesu alitupenda, na
ukitazama Ekaristi Takatifu unatambua ni kwa jinsi ghani Yesu ananipenda sasa”
(Mt. Teresa wa Kolkota). Je, wakati tunautazama mkate wa uzima, tunatambua
tunamtazama Mungu? Leo tunaalikwa tutafakari na kutambua sio tuu vipaji vya
ajabu tulivyopewa bali tuangalie wema na unyenyekevu wa yule aliyejitoa
mwenyewe.
Katika sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tufufue tena
Imani yetu juu ya uwepo wa kweli wa Yesu katika Ekaristi Takatifu. Imani hii
itujalie na kutusukuma kila wakati tuende kanisani kila jumapili tukiwa na
furaha na hamu ya kukutana na Yesu ili maadhimisho ya Ekaristi yaweze kuwa
yenye uhai na kweli nakuleta maana mbele ya Mungu. Kama kila wakati tutakuwa na
haya mioyoni mwetu, itatusaidia kujitayarisha vyema- kimwili, kiakili na
kiroho, ili tuweze kuadhimisha tukiwa wenye uchangamfu na kushiriki kikamilifu
kwenye misa, nakumpokea Yesu katika komunyo Takatifu tukiwa tunastahili. Na
hapo maadhimisho ya Ekaristi yataacha kuonekana kama tendo linalotuchosha
nakuchukua muda wetu. Badala yake linakuwa kwetu kiini, chanzo na kilele cha
maisha yetu kama Wakristo.
Sala: ninakuabudu wewe Mungu uliye jificha kweli katika Ekaristi, katika
maumbo ya mkate na divai. Moyo wangu wote unajikabidhi kwako, kwa kukutafakari
wewe unajikabidhi kwako. Asante Bwana kwakungarisha maisha yangu kila siku kwa
chakula cha malaika. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment