MASOMO YA MISA, JUNI 11, 2023
SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU
YESU KRISTU
MWANZO:
Zab. 80:17
Nimewalisha kwa unono wa ngano na kuwashibisha
asali itokayo mwambani.
SOMO 1
Kum. 8:2-3;14-16
Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia
ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili
akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake,
au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe
wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate
tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako
usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika
nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye
nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika
mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 147:12-15,19-20 (K) 12
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)
Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)
Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
aleluya. (K)
SOMO 2
1Kor. 10:16-17
Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si
ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?
Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote
twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
SHANG1LIO
Yn. 6:51
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka
kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:51-58
Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka
mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi
ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao
kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu
akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na
kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu
yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili
wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile
Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye
kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si
kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment