“MBEGU
ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Juni 22, 2025.
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa
Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristu
(Corpus Christi)
Mwa 14:18-20
Zab 110:1-4
Kor 11:23 -26
Lk: 9:11-17
EKARISTI-UJUMBE MKUBWA WA UPENDO WA
NYAKATI ZOTE.
Sister Muagustiniani, sister Juliana wa
Liège (Belgium) alipata maono ya kanisa likiwa chini ya mwezi unaongaa wenye
kidoti kimoja cheusi. Doti hii ikionesha kutokuwepo kwa sherehe ya Ekaristi.
Hii ilifanya baadaye kuwepo na sherehe ya Mwil na Damu ya Kristo ambayo
iliwekwa kwenye kalenda ya Litirujia ya Kanisa mwaka 1264 chini ya Papa Urban
wa IV. Je kulikuwa na haja ya kuwa na sherehe hii ya Ekaristi? Sherehe kama hii
kawaida inatupa nafasi ya pekee ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uwepo wa
Kristo kuwa nasi daima, ambaye yupo kweli katika Ekaristi Takatifu. Kwa upande
mwingine, ni wakati wetu wakutafakari fumbo hili kubwa la upendo. Ekaristi
Takatifu ni Sakramenti ambayo ni kilele cha Sakramenti zote, ndani yake
Sakramenti nyingine zote huadhimishwa, kwasababu ni “Fumbo la mafumbo yote” na
“Taji la Sakrament zote” sakramenti zote zinavishwa taji na Ekaristi Takatifu.
Katika Ekaristi Takatifu hatupokei tuu neema bali tunampokea Bwana wa
Neema.
Ekaristi Takatifu ni kilele cha sala sote
na kuabudu kwetu. Hakuna njia nyingine ya kuwasiliana na Mungu, yenye undani na
ukuu zaidi ya Ekaristi Takatifu. Hapa watu wawili (mtoaji na mpokeaji) wanakuwa
katika umoja wa kweli, (ndani yake, naye ndani mwako). Tunapaswa kusali mara
nyingi katika hali zote na sehemu yeyote kwasababu sala hizi zinatufanya
tuunganike na Bwana na kujenga umoja naye. Lakini kwakweli, hakuna sala yeyote
inayotoa muunganiko mkuu zaidi ya Ekaristi Takatifu. Hakuna yeyote wala
chochote kinachopaswa kutufanya tushindwe kuwa wamoja na Kristo, na kwa njia ya
umoja huu tupate nguvu tunayohitaji katika maisha yetu.
Jumapili hii tumekuja pamoja kuadhimisha
Ekaristi Takatifu kwa roho ya furaha na mapendo. Kwa bahati mbaya kuna baadhi
ya Wakatoliki wengi ambao hawaioni Ekaristi Takatifu katika hali tena. Idadi ya
Wakatoliki wanao shiriki adhimisho la Ekaristi jumapili, baadhi ya sehemu
inashuka kila mara. Misa sio sehemu ya maonesho, hawapati kile wanachotaka,
watu wanapenda kitu kipya kila wakati na tena pengine chenye mtizamo wanaotaka
wao. Ni ajabu utakuta Misa zinazo hudhuriwa mara nyingi ni, Jumatano ya Majivu,
Jumapili ya Matawi, Jumapili ya pasaka na Noeli kwasababu kuna vitu ninaongezwa
ndani yake kwa mfano, matawi, majivu, mishumaa nk. Wengi wanategemea Padre
aweke utani kwenye mahubiri ili afanye watu wachangamke, wengine wanataka kwaya
waimbe vizuri sana kwa sauti zenye kupendeza na pengine wacheze sana kwa
midundo ya kisasa zaidi, vifaa bora zaidi vya muziki, wengine wanataka wasomaji
wenye sauti nzuri zakupendeza masikioni mwao, viti vizuri vya kukaa, taa zenye
mwanga mzuri wa kupendeza na vifaa vizuri vya sauti. Kwa kweli, haya yote ni
mitazamo na matarajio. Mbaya zaidi, pengine wapo pia baadhi ya makuhani
wamenaswa kwenye mtego huu. Badala ya kuwapa watu anachosema Mungu, anawapa
watu wanachopenda kusikia na kuona. Kwa matokeo haya, neno la Mungu halihubiriwi
kiaminifu na katika unabii na maana halisi ya Uwepo wa Mungu inapotezwa.
Kumekuwako na ile hali ya mlalo (mwanadamu kwa mwanadamu) na kuacha ile hali ya
wima (Mungu kwenda kwa Mwanadamu) ya liturujia.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikti XVI
alikuwa akisisitiza kila wakati kwamba “Liturjia ni Tendo la Mungu”. Hatupaswi
kusahau kwamba kiini cha liturujia na maadhimisho ya Sakramenti ni Mungu na sio
mwanadamu. Aliendelea pia kusema; “Katekesi nzuri juu ya Ekarisiti ni Ekaristi
yenyewe ikiadhimishwa vizuri”. Kufahamu na kuamini kwamba Yesu yupo kweli
katika adhimisho la Ekaristi, tunapaswa wote tufanye jitihada kufanya adhimisho
hili lenye maana na furaha. Bila kusahau kwamba Ekaristi haiwi Ekaristi
kwasababu ya Imani ya padre au Muumini. Baada ya sala ya Ekaristi
(Konsekratsio) Yesu anakuwa kweli chini ya Maumbo ya mkate na divai. Uwe na
Imani au usiwe na Imani, Yesu anabaki kuwa Yesu katika maumbo hayo daima.
Tunadaiwa kuwa na Imani ili tuweze kushirikiana na neema ya Mungu lakini hata
tusipokuwa nayo haimaanishi utamzuia Yesu kuwa katika maumbo hayo. Tushirikiane
naye kwa Imani ili tupate neema.
Ni Mtakatifu Maximiliani Kolbe ambaye
aliwahi kusema kwa hakika kwamba, “Utimilifu wa Misa sio wakati wa mageuzo bali
ule umoja mtu anaoupokea wakati wa komunyo”. Tunaamini kwamba Ekaristi ni
sadaka ile ile aliyo itoa Yesu pale msalabani na sio kumbukumbu ya kihistoria
ya tukio lililopita, na kwamba mkate na divai unakuwa kweli mwili na damu ya
Kristo, na pia tunaamini kwamba Ekaristi ni sakramenti ya Upendo wa Mungu
kwetu. Sakramenti inayo adhimishwa katika Imani hiyo inatusaidia tuweze kuuona
umoja wa ndani wa mtu na Mungu. “Wakati tunatazama Msalaba, unatambua ni
kwajinsi ghani Yesu alitupenda, na ukitazama Ekaristi Takatifu unatambua ni kwa
jinsi ghani Yesu ananipenda sasa” (Mt. Teresa wa Calcuta). Je, wakati
tunautazama mkate wa uzima, tunatambua tunamtazama Mungu? Leo tunaalikwa
tutafakari na kutambua sio tuu vipaji vya ajabu tulivyopewa bali tuangalie wema
na unyenyekevu wa yule aliyejitoa mwenyewe.
Katika sherehe hii ya Mwili na Damu ya
Bwana wetu Yesu Kristo, tufufue tena Imani yetu juu ya uwepo wa kweli wa Yesu
katika Ekaristi Takatifu. Imani hii itujalie na kutusukuma kila wakati tuende
kanisani kila jumapili tukiwa na furaha na hamu ya kukutana na Yesu ili
maadhimisho ya Ekaristi yaweze kuwa yenye uhai na kweli nakuleta maana mbele ya
Mungu. Kama kila wakati tutakuwa na haya mioyoni mwetu, itatusaidia
kujitayarisha vyema- kimwili, kiakili na kiroho, ili tuweze kuadhimisha tukiwa
wenye uchangamfu na kushiriki kikamilifu kwenye misa, nakumpokea Yesu katika
komunyo Takatifu tukiwa tunastahili. Na hapo maadhimisho ya Ekaristi yataacha
kuonekana kama tendo linalotuchosha nakuchukua muda wetu. Badala yake linakuwa
kwetu kiini, chanzo na kilele cha maisha yetu kama Wakristo.
Sala: ninakuabudu wewe Mungu uliye jificha
kweli katika Ekaristi, katika maumbo ya mkate na divai. Moyo wangu wote
unajikabidhi kwako, kwa kukutafakari wewe unajikabidhi kwako. Asante Bwana
kwakungarisha maisha yangu kila siku kwa chakula cha malaika. Yesu, nakuamini
wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment