MASOMO YA MISA, APRILI 18, 2024
ALHAMISI, JUMA LA 3 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 8:26-40
Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia,
Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu
kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa
Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu
ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea,
ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo,
Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio,
akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?
Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na
kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, na
kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, vivyo hivyo
yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa.
Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika
nchi.
Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba,
nabii huyu asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za
mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akakianza kwa andiko lilo
hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.
Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye
maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia
nisibatizwe? Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini,
Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho
wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake
akifurahi.
Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na
alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 66:8-9, 16-17, 20 (K) 1
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu,
Itangazeni sauti ya sifa zake;
Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai,
Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe. (K)
Njoni sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Nalimwita kwa kinywa changu,
Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulinzi wangu. (K)
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu;
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)
SHANGILIO
Yn. 20: 29
Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona, wa heri
wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:44-51
Yesu aliwaambia Wayahudi: Hakuna mtu awezaye
kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.
Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila
aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu.
Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye
kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye
yuna uzima wa milele.
Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila
mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni; mtu akila
chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa
ajili ya uzima wa ulimwengu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment