JUMA LA 3 LA PASAKA, JUMATANO
SOMO 1
Mdo 8:1-8
Siku ile kulitukia adha kuu ya kanisa lililokuwa
katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria,
isipokuwa hao mitume.
Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia
maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba,
na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.
Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko
wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri
Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo
walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu
wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi
waliopooza, na viwete wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 66:1-7 (K) 1
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake,
Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini.
(K)
Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)
Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele;
Macho yake yawaangalia mataifa;
Waasio wasijitukuze nafsi zao. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua,
nao wanifuata.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:35-40
Yesu aliwaambia: Mimi ndimi chakula cha uzima;
yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.
Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja
kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka
kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa
nisimpoteze hata mmjoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake
Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na
uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment