“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumatano, Aprili 17, 2024
Juma la 3 la Pasaka
Mdo 8:1-8;
Zab 66:1-7 (K. 1);
Yn 6:35-40.
JE, MATESO YANA KUVUNJA MOYO?
Kifo cha Stefano ni mwanzo wa mateso kwa jumuiya ya Kikristo.
Lakini mbali na kujaribu kuupunguza ujasiri wa wanafunzi wa Yesu, kifo cha
Stefano kinatia chachu na nguvu ya kuendelea kuhubiri. Kutawanyika kwa Wakristo
kulikuwa na maana ya kuhubiri neno la Mungu sehemu mbali mbali na sio kukimbia
kwa sababu ya hofu.
Injili ya leo inaendelea kufundisha jinsi gani Ekaristi itafanya
kazi, ina maana gani, na kuna umuhimu gani kwa mpokeaji wa sakramenti kama
anataka imsaidie. “hakuna hata mmoja atakaye kuja kwangu atakayeona njaa au
kuona kiu” Yesu alisema. Lakini watu walikuwa na ugumu wakumuamini Yesu
analalamika kwa upole “Ingawaje mmeniona hamtaki kuamini”. Sio kwamba walikuwa
wamemuona tu bali walikuwa wameshaona mambo wakuu aliokuwa ametenda, kutembea
juu ya maji, kuongeza mikate na samaki, kuwaponya wagonjwa na kufufua wafu.
Lakini Yesu hakatishwi tamaa na mtu. Anawahakikishia; Yote alionipa Baba
yatakuja kwangu, hakuna ambaye atakuja kwangu nimkatae.
Maneno ya Yesu ni muhimu kwani yanatuhakikishia sisi kwamba ni
wakuaminika. Ni kweli kwamba tunaweza kuja kwake na kumuamini yeye, kumkabidhi
mioyo yetu, yeye atatutendea vyema, kutujali na kututunza. Yesu anauwezo
wakutujali zaidi ya hata sisi tunavyojijali wenyewe. Tunapokumbwa na dhoruba
tusikate tamaa na kuogopeshwa na majaribu tukashindwa kumwamini.
Mt. Rosemaría Escriva anasema, "dhoruba ya mateso ni nzuri.
Ina hasara gani? Kwani jambo ambalo limekwisha kupotezwa haliwezi kupotezwa
tena. Mti ukiwa na mizizi iliyojishika chini sana, hakuna upepo uwezao kuungoa
mti wa Kanisa, labda tu matawi yake makavu yataanguka”. Basi leo tuangalie
maisha yetu kama tu matawi mabichi yaliojishika na kanisa au makavu yategemeayo
kuanguka kutoka mtini muda wowote kutokana na upepo!
Sala: Ee Bwana, Utusaidie kuishuhudia Injili na kukubali mateso
yoyote yatokanayo na shughuli hiyo. Amina.
Copyright
©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment