MASOMO YA MISA, MEI 6, 2025
JUMANNE, JUMA
LA 3 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 7:51-8:1
Stefano aliwaambia
Wakuu wa Makuhani: Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio,
sikuzote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni
vivyo hivyo. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua
wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa
mmekuwa wasaliti wake, mkamwua; ninyi mlioipokea torati agizo la malaika
msiishike.
Basi waliposikia
maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.
Lakini yeye akijaa
Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa
Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama,
naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,
wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao
miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kw amawe Stefano, naye
akiomba, akisema Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti
kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli
alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:2-3, 5, 7,
16, 20 (K) 5
(K) Mikononi mwako
naiweka roho yangu, ee Bwana.
Uwe kwangu mwamba
wa nguvu,
Nyumba yenye maboma
ya kunionkoa.
Ndiwe genge langu
na ngome yangu;
Kwa ajili ya jina
lako uniongoze, unichunge. (K)
Mikononi mwako
naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee
Bwana, Mungu wa kweli.
Bali mimi
namtumaini Bwana.
Na nishangilie,
nizifurahie fadhili zako. (K)
Umwangaze mtumishi
wako,
Kwa nuru ya uso
wako;
Uniokoe kwa ajili
ya fadhili zako.
Utawaficha katika
hema
Na mashindano ya
ndimi. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi
mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 6:30-35
Siku ile, Wayahudi
walimwambia Yesu: Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda
kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani, kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa
chakula cha mbinguni ili wale.
Yesu akawaambia,
Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali
Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana
chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.
Basi wakamwambia,
Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha
uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu
kamwe.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment