MASOMO YA MISA, MEI 11, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 5 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 15:7-21
Wakati wa Mtaguso wa Yerusalemu, baada ya hoja
nyingi Petro alisimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu
siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno
la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu,
akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala
hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi
sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo
baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa
neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao.
Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza
Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu
aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo
akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu
hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya
jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa.
Baada ya mambo haya nitarejea, nami nitaijenga
tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, nami
nitaisimamisha; ili wanada- mu waliosalia wamtafute Bwana, na mataifa yote
ambao jina langu limetajwa kwao; asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele.
Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwata-
abishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba
wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na
damu. Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake;
katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:1-3, 10 (K) 3
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. (K)
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)
SHANGILIO
Lk. 24 : 25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia
katika utukufu wake.
Aleluya.
INJILI
Yn. 15:9-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama
vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo
langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi
nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia,
ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment